Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla akizungumza na wafanya biashara wadogo wa soko la Kiloleli kata ya Ibungilo)
……………………………………………………………….
Serikali haitavumilia viongozi wa wafanya biashara wadogo maarufu kama machinga wanaokwamisha zoezi la upangaji wa wafanya biashara hao katika maeneo rasmi yaliyotengwa kwaajili ya shughuli hiyo
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala wakati wa ziara yake katika masoko nane ya manispaa ya Ilemela yaliyotengwa kwaajili ya kufanya biashara za machinga kwa lengo la kufanya tathimini juu ya zoezi la upangaji wa wafanya biashara hao ambapo imeelezwa kuwa zipo changamoto zinazokwaza baadhi ya wafanya biashara ikiwemo upangishaji na uuzwaji holela wa maeneo ya kufanyia biashara, kuficha wafanya biashara maeneo yasiyo rasmi kwa biashara, umiliki wa eneo zaidi ya moja, urasimu wa kugawa maeneo kwa baadhi ya wafanya biashara na unyanyasaji vitendo vinavyofanywa na viongozi wa baadhi ya masoko jambo ambalo linachangia kurudisha nyuma zoezi hilo
‘.. Tumepokea baadhi ya changamoto na tunaendelea kuzishughulikia, tumeambiwa tukiwaondoa maeneo yasiyo rasmi, wengine wanarudi, Sasa endeleeni muone kitachotokea, hatuwezi kuwa na utaratibu wa aina hiyo, Serikali inasema hivi, wewe unasema vile ..’ Alisema
Aidha Mhe Masala mbali na kuwapongeza wafanya biashara waliokubali na kutekeleza maagizo ya Serikali ya kwenda maeneo rasmi yaliyotengwa kwaajili ya biashara amewahakikishia wafanya biashara hao kuwa kero ya upatikanaji wa nishati ya uhakika ya Mwanga itapatiwa ufumbuzi muda mfupi ujao kwani yupo mkandarasi anaeshughulikia zoezi la ufungaji wa taa kwa masoko yote sambamba na kuelekeza shirika la umeme nchini TANESCO kufunga taa za kawaida maeneo yasiyo rafiki kwa taa za mkandarasi pamoja na kuelekeza wakala wa usafiri ardhini LATRA kuanzisha safari zitakazokatiza ndani ya masoko hayo ili kuongeza mzunguko wa watu kwaajili ya kukuza biashara
Kwa upande wa afisa masoko wa manispaa ya Ilemela Bi Bertha Baragamba amemhakikishia mkuu huyo wa wilaya kuwa atatekeleza kwa wakati maagizo yote aliyoyatoa katika ziara hiyo sanjari na kuwaomba wafanya biashara hao kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira yao ya kufanyia biashara
Bi Esther Nasoro ni mfanya biashara wa chakula soko la Buzuruga wilayani humo, Ameishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kuwapanga wafanya biashara katika maeneo rasmi sambamba na kuomba kutoruhusu wafanya biashara watawanyike upya kurudi katika maeneo yao ya awali ili kupanga mji na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi