*************************
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Doroth Gwajima, Jumanne tarehe 26 Oktoba 2021, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Kituo kipya cha Elimu ya Masafa (CDE), kilichojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia kituo cha Kuzuia na kudhibiti maradhi (CDC).
Sherehe za Uzinduzi zitafanyika katika kituo hicho kilichopo mkoani Morogoro, Wilaya ya Morogoro karibu na Mizani ya Zamani, na zitahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali,
Mashiriki ya kimataifa, uongozi wa Mkoa wa Morogoro, Chuo Kikuu Mzumbe na Mwakilishi Mkazi wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Maradhi cha Marekani CDC, Dr. Mahesh Swaminathan.
Ujenzi wa Kituo cha Elimu Masafa (CDE) Morogoro, ulianza Januari 2016, kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Maradhi (CDC). Lengo la Kituo hicho ni kuendelea kutoa mafunzo yenye ubora kwa wafanyakazi wa Afya waliopo kazini, kwa njia ya masafa kupitia mtandao na Mafunzo ya ana kwa ana.
Kituo hiki kitapanua wigo, uratibu, maendeleo na kutekeleza mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Afya wa kutoa mafunzo ya masafa na kutekeleza mipango ya elimu kwa walengwa kufikia Viwango vya Kitaifa.
Kupitia msaada uliotolewa na Kituo cha Kimataifa cha CDC, Kituo hicho kimefungwa vifaa vya kisasa vitakavyowezesha mafunzo kwa njia ya mtandao kuendeshwa nchi nzima, kutumia teknolojia kuendesha mikutano kwa njia ya video, pamoja na kujenga mfumo wa utunzaji kumbukumbu kwa kozi za masomo ya kielektroniki zitakazokuwa zinatolewa.
Wadau wengine walioshiriki kwa karibu kufanikisha kukamilika kwa utendaji wa kituo hicho ni Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na Shirika la Sayansi ya Usimamizi wa Afya (MSH) ambao kwa kiasi kikubwa wameshiriki katika kuandaa mitaala ambayo itasadia kufikiwa malengo ya Kituo ya utoaji huduma za Afya zenye ubora kwa watoa huduma na wadau wa afya nchini kote.
Hadi sasa Kituo cha Elimu Masafa kimenufaisha wataalamu wa Afya takribani 34,357, hivyo kukamilika kwa jengo la Kituo hicho kutaongeza idadi ya wanufaika.
Mashirika mengine yanayotazamiwa kushiriki sherehe hizo ni pamoja Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Shirika la Idadi ya Watu Ulimwenguni (UNFPA), Shirika la Menejimenti na Maendeleo ya Afya (MDH), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Benjamin Mkapa Foundation, I-Tech Tanzania, Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto (UNICEF), JHPIEGO, Mfuko wa Kimataifa (Global Fund), Amref, CRS, CSSC, PATH, Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania na wadau wengine mbalimbali wanaotoa huduma za Afya nchini.