Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa David Msuya alipomtembelea kiongozi huyo mstaafu nyumbani kwake Upanga Jijini Dar es salaam. Oktoba 25,2021.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa David Msuya alipomtembelea kiongozi huyo mstaafu nyumbani kwake Upanga Jijini Dar es salaam. (kushoto kwa Msuya ni mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango) Oktoba 25,2021.
**************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango, leo Oktoba 25, 2021 amemtembelea na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu mstaafu Cleopa David Msuya nyumbani kwake Upanga Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais amefika Nyumbani kwa Msuya ili kumjulia hali pamoja na kupokea ushauri na busara kutoka kwa kiongozi huyo aliyehudumu tangu serikali ya awamu ya kwanza hapa nchini. Makamu wa Rais amempongeza Waziri Mkuu mstaafu Msuya kwa mchango wake alioutoa katika ujenzi wa taifa katika nyadhifa mbalimbali alizotumikia.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya ameipongeza serikali inayoongozwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza miradi ya kimkakati ilioanzishwa katika serikali ya awamu ya tano. Amesema ni muhimu miradi hiyo ikakamilika kama ilivyopangwa hapo awali ili kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka.
Aidha Msuya ameongeza kwamba ni muhimu serikali pamoja na chama tawala kushirikiana kwa pamoja na kwa karibu katika kuwaletea wananchi maendeleo ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watanzania. Amesema serikali ni vema kuendelea kuwa na uthubutu katika kuanzisha na kutekeleza miradi yenye tija kwa taifa.
Msuya ameshauri kuwepo kwa mawasiliano ya simu mahususi katika ofisi ya Rais au Makamu wa Rais ambayo wananchi wanaweza kutoa changamoto zao mojamoja hususani zile za utekelezaji wa hukumu zinazotolewa na Mahakama hapa nchini.
Katika hatua nyingine Msuya ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwahudumia vema viongozi waliomaliza muda wao hususani katika masuala ya matibabu mbalimbali wanayohitaji kuyapata ndani na nje ya nchi.
Makamu wa Rais amemuhakikishia Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya kwamba serikali inathamini mchango wa watangulizi wao katika uongozi na itaendelea kutumia busara na ushauri wa viongozi hao katika kuliletea taifa maendeleo.