*****************************
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, imetenga zaidi ya bilioni 43.242.4 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara za mkoa wa Pwani.
Bajeti hii ni mara nne ya ongezeko ya bajeti ya awali ambapo mwaka wa fedha 2020/2021 kulikuwa na sh.bilioni 12.152.160.407.3 na bajeti ya sasa 2021/2022 ni sh
bilioni 43.242.4 ikiwa ni ongezeko la asilimia 258.
Akizungumzia bajeti hiyo iliyowasilishwa na Meneja wa TARURA Pwani ,Leopold Runji katika hafla ya kusaini mikataba ya ujenzi wa kazi ya mikataba 17 kati ya mikataba 74 kwa mwaka huu wa fedha,mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge alikemea kazi za ubabaishaji kwa baadhi ya wakandarasi hususan wazalendo .
Aidha aliwaagiza wakandarasi waliopata tenda hizo, waende wakafanyekazi masaa 24 usiku na mchana ili kukamilisha miradi kwa wakati .
“Matarajio yangu ni kwamba muwe tofauti na wakandarasi wababaishaji ,wapo ambao huwa wakisaini baada ya hapo mbwembwe nyingi ,naomba tushirikiane kukiwa na tatizo mseme ili tusikwame ,”
“Na asitokee mtu kuomba pesa eti kaagizwa na mkuu wa mkoa “msikubaliane na Hilo ,na asitokee mtu akawakwamisha “
“Naomba tufanye haya Kama timu moja na asije mtu akasema nimemtuma pesa ama kafanikisha nyie kufikia hapo ,sitowavumilia kwa hili “Na mfanye kazi kikamilifu ili mmalize kwa muda mliokubaliana katika mkataba “alifafanua Kunenge.
Kunenge aliwataka mameneja wa TARURA na viongozi was vijiji ,kata , Wilaya kuliko na miradi ya ujenzi kusimamia miradi hiyo na kuimarisha ulinzi .
Mkuu huyo wa mkoa alibainisha hatosita kufika katika maeneo ya mradi wakati wowote kwa ufuatiliaji.
Pamoja na Hilo, Kunenge aliiasa jamii kulinda miundombinu ya miradi mikubwa na midogo pasipo kuihujumu na hatomvumilia yeyote atakaebainika kuhujumu .
“Namshukuru na kumpongeza Rais Samia ,Pwani ya Samia inafunguka ,Tunashuhudia ambavyo anavyofungua nchi, barabara za ndani zikifunguka na Maeneo ya pembezoni pia kwa ongezeko la fedha ya TARURA,”alisisitiza Kunenge.
Awali akitoa taarifa ya miradi inayoingia kwenye mikataba iliyosainiwa ,Meneja TARURA Pwani, Leopold Runji alieleza,kwa kipindi Cha robo ya Kwanza na ya pili kutakuwa na jumla ya mikataba 74 yenye thamani ya bilioni 17.279.736.077.11 kati ya hiyo ,mikataba 17 yenye thamani ya bilioni 6.274.607.400 imesainiwa.
Alibainisha hadi sasa TARURA Pwani imeshapokea kiasi Cha sh.bilioni 2.296.080.272.49.
Runji alisema ,ongezeko la bajeti ya mwaka huu inaenda kuongeza urefu wa barabara za lami kutoka kilometa 57 za sasa mpaka kufikia kilometa 74 sawa na ongezeko la kilometa 17 ambalo ni zaidi ya asilimia 29 kwa mwaka mmoja was fedha 2021/2022.
Pia barabara za changarawe zenye urefu wa kilometa 300 zitajengwa na kufanya ongezeko la asilimia 58 kutoka kilometa 516.6 hadi kufikia kilometa 816.62 ifikapo Juni 2022 vilevile makaravati 127 na madaraja matatu yatajengwa.