Mmoja wa wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la
Manguanjuki, Kata ya Mandewa mkoani Singida kwa niaba ya wenzake akiwasilisha
malalamiko mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya chama hicho Kata ya Mandewa,
(hawapo pichani) dhidi ya viongozi wao wa chama ambao pamoja na mambo mengine,
wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya uongozi kwa mujibu wa Katiba ya CCM,
ikiwemo kushindwa kuitisha mikutano halali ya chama kwa mfululizo wa miaka
minne tangu walipochaguliwa.
Katibu wa CCM Kata ya Mandewa, Yusuph Makera Kijanga
akizungumza na wazee hao kwenye mkutano huo.
**********************
Na Mwandishi Wetu Singida
WAZEE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Manguanjuki Kata
ya Mandewa Manispaa ya Singida wameiomba Kamati ya Siasa ya CCM ndani ya kata
hiyo kuwaondoa mara moja viongozi wa chama hicho ndani ya tawi hilo-Mwenyekiti Abdalah
Kitiku na Katibu wake Jasta Kiwigah ambao pamoja na mambo mengine, wameshindwa
kutekeleza majukumu yao ya uongozi kwa mujibu wa Katiba ya CCM, ikiwemo kushindwa
kuitisha mikutano halali ya chama kwa mfululizo wa miaka minne tangu
walipochaguliwa.
Wakizungumza mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya
kata hiyo, wazee hao wameomba maamuzi ya haraka yachukuliwe ili kunusuru uhai
wa chama kwenye maeneo hayo kutokana na viongozi hao kuonesha dhahiri ukiukwaji
mkubwa wa kanuni na taratibu za chama, sanjari na kutokuwa na mahusiano mazuri
baina yao na viongozi wa serikali ya kijiji na wananchi
Akizungumza baada ya kupokea malalamiko hayo, Mwenyekiti wa
CCM Kata ya Mandewa Hamis Ireme kwa niaba ya kamati hiyo, alisema amepokea
malalamiko ya wazee hao na kuahidi kuitisha mkutano wa wanachama ili kuangalia
uwezekano wa kukaimisha nafasi hizo.
“Kamati ya siasa ya kata baada ya kupokea malalamiko ya
wazee na kujiridhisha tumekubaliana kukutana na wanachama ili kujadiliana juu
ya jambo hilo kwa kuangalia uwezekano wa kukaimisha nafasi za Mwenyekiti na Katibu,
lengo ni kuleta ustawi na kuchagiza maslahi mapana ya chama na wanachama wetu
ndani ya tawi la Manguanjuki,” alisema Ireme.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Kata ya Mandewa, Yusuph
Makera Kijanga alisema kamati hiyo inatarajia kuitisha mkutano mkuu wa
wanachama mapema mwezi Novemba mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine, jambo
hilo lililojitokeza litatolewa taarifa ili kupata baraka juu ya mabadiliko yoyote
yanayoweza kufanyika.
Aidha, Kijanga aliwataka viongozi wengine wa matawi ndani ya
kata hiyo kuwajali, kuwapenda, kuwasikiliza na kuwa karibu na wanachama na
wananchi wote kwa kuonesha mshikamano ili kwa umoja na pamoja kuwezesha CCM
kutekeleza Ilani yake kikamilifu.
“Hii Kata ya Mandewa ni kubwa sasa kama hatutashikamana
pamoja tutachelewesha maendeleo. Na nisisitize hakuna aliye juu ya chama,
yeyote mwenye dhamana ya chama ndani ya kata yetu atakayekwenda kinyume ajue
ataharibikiwa yeye kabla hajakiharibu chama chetu,” alisema Kijanga.