Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi, Gerald Mwaitebele (kulia) akimkabidhi Sheria ya Maadili na Kanuni za Maadili, Diwani wa Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Mhe. Victor Thobias Mmanywa baada ya kuapishwa leo Jumamosi Oktoba 23,2021.
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi, Gerald Mwaitebele amekabidhi Sheria ya Maadili na Kanuni za Maadili kwa Diwani wa Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Mhe. Victor Thobias Mmanywa huku akiwataka madiwani wote nchini kuwa waadilifu kwa kuzingatia Sheria na kanuni za maadili ya uongozi.
Mwaitebele amekabidhi Sheria na Kanuni hizo za maadili leo Jumamosi Oktoba 23,2021 wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga kilichokwenda sanjari na kumuapisha Victor Thobias Mmanywa kuwa Diwani wa kata ya Ndembezi aliyechaguliwa hivi karibuni kufuatia kifo cha aliyekuwa Diwani wa kata hiyo, David Mathew Nkulila ambaye pia alikuwa Meya wa Manispaa hiyo.
Akizungumza baada ya zoezi la uapisho, Mwaitebele amewasisitiza viongozi wa umma kufuata sheria, kanuni na taratibu na kutatua migogoro katika jamii badala ya kusubiri mpaka viongozi wa ngazi za juu wafike kutatua migogoro kwenye maeneo yao.
“Msafara wa mamba na kenge wapo,kuna baadhi ya watu imekuwa ni ajabu kusikia kiongozi amekula kiapo na kusaini kiapo lakini akienda anafanya kinyume na vile alivyoapa. Ni aibu kuona diwani na diwani wanapigana hadharani, si mmesikia? Hivi ni kweli kiongozi unapigana hadharani..Nitoe agizo, nitoe angalizo kwa viongozi kuzingatia sheria na maadili ya uongozi. . Ni lazima muwe msaada kwa jamii, muwe vioo kwa jamii”,amesema Mwaitebele.
“Kuna watu ambao ni chanzo cha migogoro mfano Mheshimiwa Diwani anaingilia taratibu za wataalamu, anaingilia taratibu za manunuzi, lakini wapo watumishi wana vibanda vya biashara lakini hawataki kulipa kodi ”,ameongeza.
Aidha ameagiza viongozi kusimamia vizuri Fedha zilizotolewa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kwamba yeyote atakayethubutu kuzichakachua atashughulikiwa.
“Mhe. Rais Samia ametoa fedha lakini wapo watu ambao siyo waadilifu wanazitolea macho, niwaambie sisi tupo nyuma tunafuatilia, ikibainika, ikithibitika tutashuka nao jumla jumla”,amesema Mwaitebele.
“Naomba tufanye kazi kwa maslahi ya umma, umepewa nafasi hii siyo kwamba unafaa sana, kuna wenye akili kuliko wewe,kuna wenye uwezo kuliko wewe lakini kwa kipindi hiki umepewa nafasi hii ufanye kwa niaba,ukiondoka wewe utaacha nini cha kukumbukwa? Uongozi ni kijiti cha kupokezana leo ni wewe kesho mwingine, tunataka ukiondoka tukukumbuke kwa mema, Kiongozi unatakiwa kuwa mfano kwa jamii siyo kuwa kiongozi kero kwa jamii”,ameeleza.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Diwani wa kata ya Ndembezi, Victor Thobias Mmanywa amesema atashirikiana na Chama Cha Mapinduzi , Wananchi , Wataalamu wa Halmashauri na Madiwani katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Ndembezi huku akiahidi kuendeleza mazuri yote yaliyoachwa na marehemu David Nkulila.
Naye Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa wa Shinyanga (Serikali za mitaa),Alphonce Kasanyi amempongeza Victor Thobias Mmanywa kuapishwa kuwa diwani wa Kata ya Ndembezi kuzingatia viapo vyao akieleza kuwa ukiviishi viapo ni kazi rahisi kuongoza lakini ukikengeuka ni kazi ngumu.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amewataka madiwani na wataalamu kusimamia kikamilifu fedha zinazotolewa na serikali na kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye ujenzi wa miradi ikiwemo kusomba maji na kuchimba misingi ya majengo ya madarasa na vituo vya afya.
“Fedha zilizotolewa na Rais Samia ni Sumu, msifanye masihara naomba madiwani,Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na wataalamu wa halmashauri mhakikishe mnasimamia fedha zilizotolewa na serikali. Tayari tumepokea shilingi Milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na zingine shilingi milioni 180 kwa ajili ya shule shikizi”,amesema Mboneko.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Jomaari Mrisho Satura amesema miongoni mwa vipaumbele katika Manispaa hiyo ni pamoja Elimu na afya, ukuzaji uchumi na kuangalia makundi maalumu, suala la mipango miji na usafi wa mazingira.
Nao Madiwani wa kata ya Kizumbi , Reuben Kitinya na Mariam Nyangaka wametumia kikao hicho kueleza changamoto ya fisi kuvamia makazi ya watu na kuua watu hali ambayo inaleta hofu hivyo kuwaomba viongozi wa serikali kuingilia kati na kufanya Operesheni ya kuua fisi.
Kufuatia changamoto hiyo Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko amesema tayari serikali kwa kushirikiana na jamii imechukua hatua mbalimbali kutatua changamoto ya wanyama aina ya fisi kwa kutumia mbinu mbalimbali.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Kushoto ni Victor Thobias Mmanywa akila kiapo kuwa Diwani wa Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga leo Jumamosi Oktoba 23,2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa Lewis Kalinjuna Manispaa ya Shinyanga. Kulia ni Kamishna wa Viapo Josephat Mushi. Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Diwani wa kata ya Ndembezi Mhe. Victor Thobias Mmanywa akila kiapo cha Uadilifu baada ya kuapishwa kuwa Diwani wa Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga leo Jumamosi Oktoba 23,2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa Lewis Kalinjuna Manispaa ya Shinyanga. Kulia ni Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi, Gerald Mwaitebele.
Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Esther Makune akizungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga kilichokwenda sanjari na kumuapisha Victor Thobias Mmanywa kuwa Diwani wa kata ya Ndembezi aliyechaguliwa hivi karibuni kufuatia kifo cha aliyekuwa Diwani wa kata hiyo, David Mathew Nkulila. Kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Jomaari Mrisho Satura
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Agnes Bashemu akimkabidhi Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Diwani wa kata ya Ndembezi Mhe. Victor Thobias Mmanywa (kulia).
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Jomaari Mrisho Satura akizungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga
Diwani wa kata ya Ndembezi Mhe. Victor Thobias Mmanywa akizungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga
Madiwani na wageni waalikwa wakiwa kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga kilichokwenda sanjari na kumuapisha Victor Thobias Mmanywa kuwa Diwani wa kata ya Ndembezi aliyechaguliwa hivi karibuni kufuatia kifo cha aliyekuwa Diwani wa kata hiyo, David Mathew Nkulila.
Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi, Gerald Mwaitebele akizungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga
Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa wa Shinyanga (Serikali za mitaa),Alphonce Kasanyi akizungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga
Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog