***********************
Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam akitokea Zanzibar na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla. Mhe. Ndayishime ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb).
Mara baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam, Mhe. Ndayishimiye alielekea katika Stesheni ya Pugu na kapata taarifa fupi kuhusu mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayojengwa kutoka Dar es Salaam – Morogoro, Morogoro – Makutupora na Mwanza – Isaka ikiwa ni jumla ya Kilomita 1063 za njia kuu na njia za kupishania.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli, Bw. Masanja Kadogosa amemueleza Mhe. Ndayishimiye kuwa hadi sasa ujenzi wa SGR (kipande cha Pugu – Morogoro) umefikia asilimia 94 na kuwa unaendelea vizuri.
Aidha, mara baada ya kupata taarifa fupi kuhusu mradi wa ujenzi wa SGR, Mhe. Rais Ndayishimiye ametembelea bandari kavu eneo la Kwala Mkoani Pwani.
Mhe. Ndayishimiye amesema kuwa eneo la bandari kavu (Kwala) litakuza biashara kati ya Tanzania na Burundi na litatusaidia kupunguza gharama za usafiri na fedha zitakazookolewa zitaenda kwenye miradi mingine.
“Mradi huu pia utapunguza gharama za bidhaa mbalimbali Nchini Burundi, kwetu sisi Burundi, mtu akikupa eneo amekuthamini sawa na kukuunga undugu kwenye familia yake,” amesema Mhe. Ndayishimie.
Awali akitoa taarifa ya eneo hilo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Mb) amesema eneo hilo lina ukubwa wa hekta 502, kati ya hizo hekta 10 zimetengwa kwa ajili ya Serikali ya Burundi.
“Dhumuni la kutenga eneo hili ni kupunguza msongamano wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam,” Amesema Prof. Mbarawa na kuongeza kuwa ujenzi wa miundombinu ya eneo hili utakapokamilika utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 37.23.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya NJe na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema kuwa kupitia mradi wa ujenzi wa bandari kavu eno la Kwala utasaidia kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Burundi pamoja na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.