Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Viongozi mbalimbali wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ujamaa Umwe Kusini Ikwiriri Wilayani Rufiji Mkoani Pwani kwa ajili ya kuhudhuria Maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania UWT
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia katika Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) iliyoambatana na kumbukizi ya Kumuezi Bibi Titi Mohammed Mwenyekiti wa kwanza wa UWT. Maadhimisho hayo yamefanyika leo tarehe 23 Oktoba, 2021 katika Uwanja wa Ujamaa Umwe Kusini Ikwiriri Wilayani Rufiji Mkoani Pwani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, hayupo pichani akipokea maandamano katika Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) iliyoambatana na kumbukizi ya Kumuezi Bibi Titi Mohammed Mwenyekiti wa kwanza wa UWT. Maadhimisho hayo yamefanyika leo tarehe 23 Oktoba, 2021 katika Uwanja wa Ujamaa Umwe Kusini Ikwiriri Wilayani Rufiji Mkoani Pwani.
Baadhi ya washiriki wakifatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,(hayupo pichani) wakati akihutubia Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) iliyoambatana na kumbukizi ya Kumuezi Bibi Titi Mohammed Mwenyekiti wa kwanza wa UWT. Maadhimisho hayo yamefanyika leo tarehe 23 Oktoba, 2021 katika Uwanja wa Ujamaa Umwe Kusini Ikwiriri Wilayani Rufiji Mkoani Pwani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiagana na Viongozi mbalimbali wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mara baada ya kuhutubia katika Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) iliyoambatana na kumbukizi ya Kumuezi Bibi Titi Mohammed Mwenyekiti wa kwanza wa UWT katika Uwanja wa Ujamaa Umwe Kusini Ikwiriri Wilayani Rufiji Mkoani Pwani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza jambo na Mwenyekiti wa UWT Mama Gaudensia Kabaka baada ya kuhutubia katika Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) iliyoambatana na kumbukizi ya Kumuezi Bibi Titi Mohammed Mwenyekiti wa kwanza wa UWT katika Uwanja wa Ujamaa Umwe Kusini Ikwiriri Wilayani Rufiji Mkoani Pwani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Msanii Ikuzi Kicheko (Mzalendo Halisi) baada ya kuonesha usanii wake kwenye Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) iliyoambatana na kumbukizi ya Kumuezi Bibi Titi Mohammed Mwenyekiti wa kwanza wa UWT katika Uwanja wa Ujamaa Umwe Kusini Ikwiriri Wilayani Rufiji Mkoani Pwani
PICHA NA IKULU
……………………………………………………………………..
RAIS Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM ametoa maagizo matatu kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika kuelekea kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru Desemba 9 mwaka huu.
Maagizo hayo ni pamoja na kutoa taarifa ya hali ya kiuchumi kwa Wanawake nchini, hali ya kisiasa kwa wanawake nchini pamoja na taarifa ya namna ambavyo Wanawake wamekombolewa kifikra nchini.
Rais Samia ametoa maagizo hayo leo wilayani Rufiji mkoani Pwani wakati akizungumza katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya UWT kitaifa ambapo alialikwa kuwa mgeni rasmi.
Ameitaka UWT kukaa na Taasisi ya ULINGO na kuandaa mkutano mkubwa kabla ya maadhimisho ya Sikukuu ya Uhuru na kueleza ni kwa kiasi gani wamefanikiwa kumkomboa Mwanamke kifikra, kiuchumi na kisiasa tokea Uhuru.
Amesema lengo la kuanzishwa kwa UWT ilikua ni kuwakomboa Wanawake wa kitanzania kwenye nyanja mbalimbali hivyo ni vema wakaja na taarifa inayoeleza mafanikio ambayo wameyapata katika kuwainua Wanawake.
” UWT ilianzishwa kwa lengo la kuwakomboa Wanawake kifikra, kiuchumi na kisiasa, na hii ndio kauli mbiu ya maadhimisho yetu mwaka huu, hivyo niwatake UWT na ULINGO kuandaa mkutano mkubwa utakaogusia taarifa ya hali ya mwanamke katika nyanja hizo,” Amesema Rais Samia.
Ameipongeza Jumuiya hiyo kwa kuwa sehemu ya Jumuiya zilizochangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha viongozi wakubwa wanawake ambao wameitumikia Tanzania na nje ya Nchi kwa mafanikio makubwa.
” Jumuiya yetu imekua kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kuzalisha viongozi bora ambao wameitumikia Nchi yetu ndani na nje ya Nchi, niwaombe kuendelea kuzalisha viongozi zaidi.
Kwa muda mrefu Wanawake tumekua tukisaidia wanaume kushika hatamu za uongozi tokea enzi za Bibi Titi Mohamed hadi sasa kwa kudra za Mwenyezi Mungu tumeshika hatamu sisi wenyewe,” Amesema Rais Samia.
Akizungumzia Bibi Titi Mohamed, Rais Samia amesema Bibi Titi alikua ni mwanamke shupavu na shujaa ambaye alimsadia kwa kiasi kikubwa Baba wa Taifa Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere katika mapambano ya kudai Uhuru.
” Niwaombe Wanawake wote mlioko hapa tutoke tukiwa na moyo shupavu kama wa Bibi Titi, twendeni pamoja tukalitumikie kwa Taifa letu,” Amesema Rais Samia.
Rais Samia pia ameipongeza UWT kwa kufanikiwa kubadilisha mitazamo ya Wanawake na kuwa chanya, kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali za kijasiriamali sambamba na elimu ambapo wamekua na Shule zao ambazo zimekua zikichangia ukuaji wa kiwango cha elimu nchini.
” Pamoja na mambo mengine niwapongeze UWT kwa kusimama na Chama chetu Cha Mapinduzi CCM kwa Miaka yote, UWT imekua sehemu ya mafanikio ya CCM ni wazi CCM ni Wanawake na Wanawake ni CCM, tuendelee kuchapa kazi,” Amesema Rais Samia.
Pia ametoa wito kwa Wanawake wote kutoka na kauli mbiu moja yenye lengo la kupinga kwa nguvu tabia ya unyanyasaji na matukio ya ukatili wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto nchini.
” Niwaombe wote kutoka na kauli moja ya kupinga tabia za ukatili kwa Wanawake na Watoto, ni ukweli kuwa wanawake tumekua tukichangia vitendo hivi kwa kutototoa taarifa kwenye vyombo husika au kuunga mkono vitendo hivyo tu kwa sababu aliyefanyiwa siyo Ndugu yako ama Mtoto wako,” Amesema Rais Samia.
Tukio la kilele hicho cha wiki ya Wanawake kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali akiwemo Naibu Katibu Mkuu Bara, Christina Mdeme, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, Mawaziri, Wabunge na Madiwani.