************************
Na John Mapepele, Morogoro
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Dkt. Philip Isdor Mpango amezitaka Wizara, Idara na Mikoa ambayo haijashiriki kwenye Michezo ya Wafanyakazi ya Wizara na Idara za Serikali SHIMIWI ya mwaka huu kutoa maelezo ya kina kwa Mhe.Waziri Mkuu kuhusu sababu za kushindwa kushiriki na nakala yake ipelekwe kwa Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ndiye mlezi wa mashindano hayo.
Dkt Mpango ametoa maagizo hayo leo, Oktoba 23, 2021 mjini Morogoro wakati alipokuwa akifungua michezo hiyo ya SHIMIWI ambapo amesisitiza kuwa michezo hiyo inapaswa kuwa endelevu kwa watumishi wote wa Serikali wakati wote badala ya kusubiri mashindano SHIMIWI yanayofanyika katika kipindi kifupi ili kuimarisha afya na kujikinga na magonjwa mbalimbali.
Aidha, amesema anatambua jitihada zinazofanywa na Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo katika kuendeleza na kuboresha michezo nchini na ameiagiza Wizara ishirikiane na uongozi wa SHIMIWI kufanya tathmini ya mashindano ya mwaka huu ambapo ametaka kufanywa kwa tathimini kwa kila timu na kuja na mikakati ya kuboresha mashindano haya katika miaka ijayo.
Ameonya tabia ya kukimbilia kuandaa timu za michezo kwa muda mfupi kabla ya mashindano na kueleza kuwa hayo ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali na kuna madhara makubwa kwa kufanya hivyo.
“Hayo ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali, mnaandaa timu wiki mbili kabla ya mashindano ili kupata posho tu. Acheni kufanya hivyo”.Ameonya Dkt. Mpango
Amewataka wanamichezo wote kuwa nidhamu katika kipindi chote cha mashindano haya na kuonya kuwa yoyote atakaye bainika achukuliwe hatua kali.
“Ninyi ni watumishi muwe na maadili na nidhamu ya hali ya juu, sitegemei utovu wa nidhamu, michezo ya SHIMIWI siyo sehemu ya kufanya uzinzi na ulevi lakini pia nawakumbusha UKIMWI upo”. amesisitiza Mhe. Mpango
Ameitaka Wizara na uongozi wa SHIMIWI kujiridhisha na wachezaji ambao siyo watumishi (mamluki) ambapo amesema wakiwabaini adhabu kali kwa wahusika na timu husika ili liwe fundisho.
Ametoa rai kwa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kuyafanya mashindano haya kuwa endelevu na kubaini vyanzo mbalimbali ya mapato ambayo vitasaidia kuyafanya mashindano hayo kuendelea kufanyika katika ubora.
Kuhusu baadhi ya waajiri kutowaruhusu wafanyakazi kushiriki kwenye michezo hiyo kwa kisingizio cha fedha na muda. Mhe Mpango ameelekeza Wizara, Mikoa na Idara zote za Serikali kuhakikisha bajeti kwa ajili ya kichezo zinatengwa mapema na waajiri wawaruhusu watumishi kufanya mazoezi kwa muda mwafaka.
Aidha ameyaagiza mashirikisho ya michezo nchini kushirikiana kikamilifu na Wizara yenye dhamana na michezo ili kuboresha michezo badala ya mashirikisho hayo kuandaa mikakati yao bila kushirikisha Wizara mama.
Pia ameziagiza Wizara, Idara , Taasisi na Mikoa kuweka utaratibiu wakufanya mazoezi japo mara moja kwa wiki na amezipongeza mamlaka ambazo tayari zimejipangia utaratibu wa kufanya mazoezi ambapo amefafanua kuwa michezo siyo tu inasaidia kutoa ajira na kukuza uchumi bali inasaidia kujenga afya kwa kupunguza magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, moyo na figo.
Amesema mwaka 2016 takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 71% ya vifo vyote nchini vilitokana na magonjwa yasiyoambukizwa ambayo yangeweza kutibika na kupunguza vifo hivyo kwa kufanya mazoezi.
Akizungumzia ushiriki wa Zanzibar kwenye SHIMIWI amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo kuwasiliana mara moja na Waziri mwenye dhamana ya Muungano kwa upande wa Zanzibar ili waweze kushiriki kwenye michezo ijayo.
Kuhusu chaguzi za viongozi wa mashirikisho zinazotarajiwa kufanyika hivi karibuni ametoa wito wa kuwachagua kwa mujibu wa katiba viongozi bora ambao wataendeleza michezo kulingana na Sera ya Michezo ya Mwaka 1995 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi yam waka 2020.
Aidha ameitaka Wizara kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kusimamia kanuni kwenye eneo la uongozi bora kwenye mashirikisho ya michezo hapa nchini.
Akijibu maombi ya uongozi wa SHIMIWI kuhusu Serikali kusaidia kujenga miundombinu ya michezo na vifaa kwa watumishi amewataka kuwasilisha hoja hizo kwa Katibu Mkuu wa Sanaa, Utamaduni na Michezo ili zishughulikiwe.
Akizungumzia Tamasha la Michezo kwa Wanawake la Tanzanite lililoandaliwa na Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo hivi karibuni amepongeza jitihada hizo na kuiagiza Wizara liandaliwe vizuri zaidi katika mwaka ujao ili muasisi wa Tamasha hilo ambaye ni maono ya Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania aweze kuwa mgeni rasmi.
Akifafanua amesema michezo hii ina faida nyingi ambapo amezitaja kuwa ni pamoja na kuimarisha mshikamano, kuleta umoja wa kitaifa, kuwafanya watumishi wajiamini na kuongeza uzalendo.
Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa uviko-19 Mhe. Mpango amepongeza Wizara na uongozi wa SHIMIWI kwa kuzingatia tahadhali zote katika michezo ya mwaka huu ikiwa ni pamoja na kuwa na kituo kwa ajili ya kutoa huduma ya chanjo ya hiari kwa wanamichezo ambapo pia amesisitiza wanamichezo wote kuwa mabalozi wa kukabiliana na ugonjwa huo kuanzia kwenye familia zao.
Mashindano ya SHIMIWI ya mwaka huu 2021 yameshirikisha Wizara 24, mikoa 11, Wakala 4 na Idara 8 za Serikali. Mashindano ya SHIMIWI yamefufuliwa mwaka huu kufuatia maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu aliyoyatoa Agosti 15, 2021 wakati akishiriki CRDB Marathon akimwakilisha Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano.