Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro kufungua Michezo ya 35 ya SHIMIWI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akipokea maandamano ya timu mbalimbali kutoka Wizara, Mikoa na Idara mbalimbali za Serikali wakati wa Ufunguzi wa Michezo ya 35 ya SHIMIWI katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akikabidhi Mpira wa mikono na Mpira wa Miguu kwa wawakilishi wa timu za mpira wa miguu na timu za mpira wa mikono wakati wa ufunguzi wa Michezo ya 35 ya SHIMIWI inayofanyika katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Washiriki wa Michezo ya 35 ya SHIMIWI katika mchezo wa kuvuta Kamba timu ya Wizara ya Fedha (wenye nguo rangi nyekundu) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania wakichuana wakati wa Ufunguzi wa Michezo ya SHIMIWI inayofanyika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro. Oktoba 23,2021.
…………………………………………………………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango, leo Oktoba 23, 2021 amefungua Michezo ya 35 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) inayofanyika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Akifungua Michezo hiyo, Makamu wa Rais ameagiza Watendaji Wakuu wa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kuhakikisha wanatenga muda kwaajili ya watumishi wa serikali kufanya mazoezi walau siku moja katika wiki. Aidha amewataka watendaji wakuu wa Wizara,Idara na Taasisi za Serikali ambazo hazijashiriki katika mashindano hayo kwa mwaka 2021 kujieleza kwa maandishi kwa Waziri Mkuu sababu za kutoshiriki kwao Michezo hiyo. Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuhakikisha bajeti za ushiriki katika michezo zinapangwa mapema, na kuruhusu watumishi kufanya mazoezi kwa muda muafaka ya kujiandaa kushiriki vizuri katika mashindano hayo kila mwaka.
Aidha Makamu wa Rais amekemea vikali ushiriki wa wanamichezo wasiowatumishi wa Umma katika Mashindano hayo. Ameitaka Wizara ya Michezo Sanaa na Utamaduni kwa kushirikiana na Uongozi wa SHIMIWI,kujiridhisha kwa kina kwamba katika mashindano hayo washiriki wote ni watumishi wa Umma na kuwachukulia hatua kali kuanzia viongozi na wote watakaobainika kushirikisha wanamichezo wasiowatumishi wa Umma katika mashindano hayo.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ametoa wito kwa wananchi wote kuendelea kushiriki katika michezo pamoja na kufanya mazoezi ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa yasioambukiza. Amesema katika taarifa ya hali ya Magonjwa yasiyoambukiza na Umaskini hapa nchini iliyotolewa mwaka 2020 na Kamisheni ya Magonjwa Yasiyoambukiza, inaonyesha kuwa, magonjwa hayo yanachangia zaidi ya asilimia 33 ya vifo vyote nchini hivyo watanzania hawana budi kuwekeza muda pia katika kushiriki michezo pamoja na mazoezi.
Pia Makamu wa Rais amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira , Selemani Jafo kuanza mapema mchakato wa kuwashirikisha watumishi wa umma wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili mwakani waweze kushiriki Michezo ya Shimiwi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) Daniel Mwalusamba amesema michezo hiyo imekuwa na faida kwa watumishi wa umma kwani imekua ikiwapa nafasi watumishi kujifunza na kubadilishana mbinu za utendaji kazi,kuondoa rushwa katika taasisi za serikali miongoni mwa watumishi kutokana na kuwakutanisha mara kwa mara katika michezo pamoja na kuondoa tabaka katika utekelezaji wa majukumu ya serikali kati ya watumishi wa ngazi za chini, kati na ngazi ya juu.
Awali Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamduni na Michezo Dkt. Hassan Abbas amesema serikali itaendelea kuboresha michezo nchini pamoja na kutambua umuhimu wa sekta hiyo katika kutoa ajira kwa watanzania. Amesema katika kuinua michezo kwa wanawake hapa nchini Wizara imeandaa Tamasha la Michezo la Wanawake litakalowawezesha kujiimarisha kimichezo huku akitoa nafasi kwa timu za wanawake zinakazofanya vizuri katika mashindano ya SHIMIWI kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo moja kwa moja.