Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax,akizungumza wakati wa sherehe za kuadhimisha Miaka 76 ya Umoja wa Mataifa (UN DAY) zilizofanyika leo Oktoba 23,2021 jijini Dodoma kwenye viwanja vya Nyerere Square.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Ziatan Milisic,akizungumza wakati wa sherehe za kuadhimisha Miaka 76 ya Umoja wa Mataifa (UN DAY) zilizofanyika leo Oktoba 23,2021 jijini Dodoma kwenye viwanja vya Nyerere Square.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka,akizungumza wakati wa sherehe za kuadhimisha Miaka 76 ya Umoja wa Mataifa (UN DAY) zilizofanyika leo Oktoba 23,2021 jijini Dodoma kwenye viwanja vya Nyerere Square.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax,akikabidhiwa cheti na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Ziatan Milisic wakati wa sherehe za kuadhimisha Miaka 76 ya Umoja wa Mataifa (UN DAY) zilizofanyika leo Oktoba 23,2021 jijini Dodoma kwenye viwanja vya Nyerere Square.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuhutubia wakati wa sherehe za kuadhimisha Miaka 76 ya Umoja wa Mataifa (UN DAY) zilizofanyika leo Oktoba 23,2021 jijini Dodoma kwenye viwanja vya Nyerere Square.
……………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Ugonjwa wa Corona (UVIKO-19) umesababisha changamoto nyingi duniani katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, uchumi, usafirishaji, maji na utalii, hivyo dunia imetakiwa kuchukua changamoto hizo kama funzo ili kujipanga upya na namna ya kukabiliana na majanga ya mlipuko.
Hayo yemeelezwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) alipokuwa anahutubia katika sherehe za kuadhimisha Miaka 76 ya Umoja wa Mataifa (UN DAY) zilizofanyika leo jijini Dodoma kwenye viwanja vya Nyerere Square.
Dkt. Tax alisema kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu “Kujijenga tena kwa kujenga mifumo ya afya bora” ni kielelezo cha wazi kuwa dunia haina budi kushirikiana ili kujenga mifumo madhubuti ya afya yenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko. Lengo la mifumo hiyo ni kuhakikisha kuwa nchi hazipati athari kubwa zinazosababishwa na majanga kama hili la mlipuko wa UVIKO-19.
Dkt. Tax aliushukuru Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano wake katika sekta mbalimbali nchini na kuuahidi umoja huo na wadau wengine wa maendeleo kuwa, Tanzania itaendelea kushirikiana nao katika kukabiliana na janga la Corona. Alifafanua kuwa Serikali itaendelea kufuata miongozo yote inayotolewa na Shirika la Afya Duniani pamoja na kujenga mfumo imara wa afya wenye kuhakikisha vituo bora vya afya, watumishi wa kutosha, vitendea kazi, dawa na miundombinu mingine ili kutoa huduma bora za afya nchini.
Alisema Serikali ilishaweka mikakati ya utekelezaji wa haya yote katika Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma hivi karibuni.
Alihitimisha hotuba yake kwa kuwahimiza wananchi kutumia fursa ya chanjo zilizopo nchini, kwa kuwa chanjo hizo zinapatikana kwa tabu na hadimu duniani.
Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Ziatan Milisic ,amesema ujumbe Mkuu wa mwaka huu katika siku ya maadhimisho ya siku ya Umoja wa Matiafa (UN) kwa kuweka ni kujijenga katika mifumo bora ya Afya,elimu mazingira ili kufikia lengo la Maendeleo Endelevu (SDGs).
“Hatuna budi kuendelea kushirikiana kuunga mkono juhudi zote za kujenga mifumo ya Afya iliyo na uhimilivu zaidi itakayo hakikisha kwamba jamii na Watu wanakuwa na Afya bora, wanapata huduma za msingi za Afya na wanaweza kuhimili majanga ya kiafya kama UVIKO-19″amesema.
Amesema tangu janga la UVIKO-19 litangazwe kuingia nchini Tanzania, Umoja wa Matiafa wamekuwa mstari wa mbele kusaidia nguzo mbalimbali katika mwitikio wa kitaifa dhidi ya janga hilo ambapo baadhi ya mashirika na Umoja wa Matiafa yakishika uwenyekiti wenza wa nguzo hizo za mwitikio.
Aidha Bw. Milisic amesema kutokana na mwitikio huo Umoja wa Matiafa wamekuwa wakishirikiana na washirika kwa kitaifa na kimataifa katika kuhakikisha kuwa huduma muhimu za Afya kama vile za akina mama, watoto na vijana baleghe,VVU/UKIMWI na ukatili wa kijinsia zinaendelea katika kipindi chote cha janga.
“Tumekuwa tukijenga na kufanya marekebisho ya kliniki na zahanati, baadhi zikiwa pembezoni mwa nchi na kuvipa vifaa vinavyohitajika ili kuhakikisha wanawake wanapata pahala pakujifungulia kwa usalama na watoto wachanga wanapata matunzo yanayostahili”amesema.