Na Joseph Lyimo
MSICHANA wa jamii ya kidatoga wa Kata ya Bassotu Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, Neema John (Udaa) siyo jina lake halisi amesema aliamua kuachana na uamuzi wa wazazi wake wa kulazimishwa kufanya kazi za ndani na kuamua kupata elimu.
Udaa anaeleza kuwa wazazi wake walitaka akafanye kazi za ndani Katesh ili awe anawatumia fedha ila alikataa na kuamua kuendelea na masomo baada ya kuhitimu darasa la saba na kuchaguliwa kuendelea na sekondari.
Anasema baadhi ya wazazi na walezi wa watoto wa eneo hilo ambao ni jamii ya wafugaji hawapendi watoto wapate elimu hiyo huwashinikiza wakafanye kazi za ndani au kuolewa ili wapewe mahari ya ngombe ila yeye aligoma.
“Mimi nina ndoto ya kuwa mwalimu hivyo baada ya kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari nilikuwa najiandaa ndipo wazazi wakaniambia nikafanye kazi za ndani Katesh ila nikakataa,” amesema Udaa.
Amesema aliwaeleza wazazi wake kuwa kuna shirika lisilo la kiserikali analolifahamu wakiendelea kumkataza asiendelee na masoko akafanye kazi za ndani atatoa taarifa ndipo wakamkubalia.
Amesema yeye binafsi ametambua haki yake ya kupata elimu ndiyo sababu aliwaeleza wazazi wake kwa kuwaambia kuwa wamuache asome la sivyo atawashitaki ndipo wakamkubalia.
“Mwamko wa wazazi wangu hivi sasa umebadilika kwani awali hawakutaka nisome ila baada ya mimi kuonyesha msimamo kuwa napenda elimu walikubali niendelee na masomo na nisiajiriwe kufanya kazi za ndani,” amesema Udaa.
Amesema baadhi ya wazazi na walezi hufanya makubaliano na watoto wao kwenda kufanya kazi za ndani au kuacha masomo ili wakaolewe na kuacha haki zao za kupata elimu ila kwake alisimama kidete.
Mratibu wa uwezeshaji jamii kisheria wa kituo cha msaada wa sheria wa wanawake na watoto, Consolata Chikoti amesema jamii inatakiwa kutoa ushirikiano, wasiwaone maadui, wajue kuwa wana nia njema ya kusaidia jamii na pia mpango kazi wa Taifa ujulikane kwa wadau wote.
“Tumeamua kuja Hanang’ na kukutana na jamii ya eneo hili kwa sababu tumeona hii jamii ina uhitaji wa aina yake, ina watoto wenye vipaji, lakini kuna vikwazo vikiwemo mila na desturi kandamizi kwa watoto wa kike na wanawake,” amesema Chikoti.
Amesema katika kukabiliana na vitendo hivi vya kikatili suala la ushahidi nalo limekuwa kikwazo, kwani sheria ina mapungufu makubwa, kuna matatizo mengine yanahitaji mbinu mbadala ikiwemo sheria yenyewe ilivyo.
“Pamoja na Serikali kupanga bajeti kutekeleza mpango huu, bado ina mambo mengi, hivyo wadau tajwa waone haja ya kuchangia kufanikisha zoezi hilo na kutokomeza kwa ajili ya manufaa ya wasichana na wanawake kwa ujumla,” amesema Chikoti.
Hivi karibuni mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere alifanya ziara kwenye wilaya mbalimbali za mkoa huo na kuwataka wazazi, walezi wenye wanafunzi kuhakikisha wanaendelea na masomo.
“Kama una mtoto anayesoma shule ya msingi au sekondari uhakikishe anahitimu masomo yake na endapo akiolewa au kukatizwa masomo yake tutawachukulia hatua kali za kisheria,” amesema Makongoro.