Na Joseph Lyimo
MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Manyara, (RMO) Dkt Damas Kayera amewataka wananchi wa eneo hilo kujitokeza na kuchanja chanjo ya kujikinga na maambukizi ya Uviko-19 na kuachana na dhana potofu zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Dkt Kayera ameyasema hayo mjini Babati akizungumza kwenye kikao cha kamati ya maafa ya mkoa huo kwa kudai kuwa jamii inapaswa kutoamini maneno pofotu ya kwenye mitandao kwani chanjo hiyo imethibitishwa ni salama.
Amesema propaganda za kuganda kwa damu mwilini baada ya kupata chanjo au kijiko kung’ang’ania mkono uliochomwa chanjo ni maneno potofu yanayopaswa kutosikilizwa kwani siyo ukweli.
Amewataka kuepuka propaganda zinazotolewa na baadhi ya watu wasiokuwa na utaalam wa afya wanaosema ina madhara kwenye mwili wa binadamu jambo ambalo siyo kweli.
Amesema chanjo hiyo ni muhimu na imefanyiwa tafiti za kisayansi na serikali imejiridhisha kupitia Wizara ya Afya na shirika la afya duniani (WHO) kuwa chanjo hiyo haina madhara.
“Chanjo ya Uviko-19 ukiipata ni kinga nzuri kwani endapo ukipata maambukizo ya Uviko-19 haitakuathiri sana kama yule mtu ambaye hakupata chanjo ambaye anapata madhara makubwa,” amesema Dkt Kayera.
Amesema watu ambao hawajachanja wakipata ugonjwa huo wanasababisha gharama kubwa kwa familia na Taifa kwa ujumla ila ukichanja na hata ukipata maambukizo hautaathirika kwa kiasi kikubwa.
Amesema ni vyema watu wakafuata ushauri wa kitaalamu na kuachana na maneno potofu ya wale ambao hawajapata elimu ya kisayansi wanavyofanya kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii.
“Mtu hana taaluma yoyote ya afya anatangaza kwa watu eti chanjo inasababisha mtu awe mnyama, msiwasikilize watu wanamna hiyo kwani ni wapotoshaji wasio na chochote,” amesema.
Mkazi wa kata ya Nangara mjini Babati, Said Maro amesema serikali inapaswa kuwachukulia hatua watu wanaosambaza taarifa za uongo kutokana na ugonjwa huu wa Uviko-19.
“Huwezi kuwapa watu hofu kwa sababu yako wewe ambao hutaki kuchanjwa kwani Serikali imesisitiza kuwa chanjo ni hiyari hivyo siyo vyema kuwaogopesha wale waliochanja,” amesema Maro.
Mkazi wa kona ya Nakwa mjini Babati John Thobias amesema yeye binafsi ameshapatiwa chanjo ya Uviko-19 kwani hakusikiliza propaganda za watu kwenye mitandao.
“Binafsi nilipatiwa chanjo kwenye hospitali ya mji wa Babati ya Mrara na sikupata tatizo lolote tangu nilipochanjwa mwezi Agosti mwaka huu, kama baadhi ya watu wanavyotutisha,” amesema Thobias.