Mwenyekiti wa Umoja wa wafanyabiasahara wadogo(wamachinga)mkoa wa Ruvuma Salum Masamaki wa kwanza kushoto na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,wakifuatilia taarifa juu ya upangaji wa maeneo kwa wamachinga hao wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa mpango wa kuwapanga wafanyabiashara wadogo(Wamachinga) katika Halmashauri za mkoa huo.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,akiongea wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa mpango wa kuwapanga wafanyabiashara wadogo(wamachinga).
Baadhi ya Maafisa Biashara kutoka Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma wakifuatilia ufunguzi wa uzinduzi wa mwongozo wa mpango wa kuwapanga wafanyabiashara katika maeneo ya kufanya shughuli zao.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia uzinduzi wa Mwongozo huo uliofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
…………………………………………………………………..
Na Muhidin Amri,Songea
WAFANYABIASHARA wadogo(wamachinga)mkoani Ruvuma, wametakiwa kutii kuheshimu za sera za nchi kwa kukubali kwenda katika maeneo waliyotengewa kufanya shughuli zao.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, amesema hayo jana wakati akizindua rasmi mwongozo wa mpango wa kuwapanga wafanyabiashara wadogo(Wamachinga) katika Halmashauri za mkoa huo.
Jenerali Ibuge, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya kuhakikisha wanatenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwa wafanyabiashara wadogo.
Ameagiza, maeneo hayo ni lazima yawe rafiki yatakayofikika na wafanyabiashara na wateja kwa urahisi na kuruhusu wamachinga kufanya shughuli zao kwa uhuru na utulivu bila kuathiri shughuli zao ili kuepuka fujo,vurugu na migogoro.
Jenerali Ibuge,amesema viongozi wa Halmashauri na wilaya wahakikishe maeneo watakayotenga kwa ajili ya Wamachinga kufanya biashara zao yanakuwa na miundombinu muhimu kama vyoo,maji na umeme.
Katika hatua nyingine Jenerali Ibuge, amewataka wakuu wa Taasisi za Tarura,Tanesco,Tanroad,Latra,Souwasa na Ruwasa ambazo ni mtambuka kushiriki vyema katika mpango huo.
Amesema, ni vyema taasisi hizo kushirikiana na viongozi wa Machinga kupanga na kutekeleza mikakati madhubuti ili sekta hiyo yenye wadau wengi inakwenda kustawi na kufanyika katika mazingira bora.
Aidha Mkuu wa mkoa,amewakumbusha viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wadogo(Machinga)waliochaguliwa kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha zoezi la usajili wa Wamachinga kwa kutumia mfumo maalum wa vitambulisho.
Ibuge, ametaka zoezi hilo lifanyike kwa ufanisi na viongozi wa Halmashauri wahakikishe kazi ya kuwapangia maeneo wamachinga ni shirikishi na jumuishi.
Mwenyekiti wa Chama cha Jumuiya ya wafanya biashara wadogo(Machinga) Salum Masamaki ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuamua kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za wajasirimali wadogo.
Amesema,wako tayari kuondoka katika maeneo yasioruhusiwa na wanayofanya shughuli zao kwa sasa na kwenda katika maeneo ambayo yatatengwa na Serikali kupitia Halmashauri za wilaya.
Hata hivyo, Masamaki ameiomba Serikali kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa rafiki kwa shughuli zao pamoja na kupeleka baadhi ya huduma muhimu kama maji,umeme,barabara ili kutoa fursa kwao kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki amesema,Mkoa wa Ruvuma unaendelea kusimamia zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya Wajasirimali wadogo.
Amesema,vitambulisho hivyo vinatolewa kupitia mfumo maalum wa ugawaji wa vitambulisho vilivyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Nchini(TRA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi.
Amesema,hadi kufikiwa tarehe 20 Oktoba 2021 mkoa wa Ruvuma umegawa vitambulisho 5,119 sawa na asilimia 9.14 ya lengo la kugawa vitambulisho 56,000.
Kwa mujibu wa Ndaki, changamoto kubwa ni ukosefu wa takwimu sahihi za Machinga waliopo katika mkoa wa Ruvuma,mwitikio mdogo wa Machinga kuchukua vitambulisho,machinga kutokuwa na sehemu moja ya kufanyia biashara.
Amesema, changamoto hizo kwa kiasi kikubwa usababisha ugumu wakati wa ukaguzi na kubaini wajasirimali wadogo wasio sajiliwa na wasio na vitambulisho.