………………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais wa awamu ya sita Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anapenda na kuthamini michezo mbalimbali nchini na atahakikisha inaendelea kushamiri na kuongeza tija.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wadau wa michezo na wanamichezo wote nchini kwamba Serikali itaendelea kuunga mkono shughuli zote za michezo ukiwemo mchezo wa mpira wa miguu.
Mheshimiwa Majaliwa aliyasema hayo jana usiku (Alhamisi, Oktoba 21, 2021) katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa wanamichezo waliofanya vizuri msimu wa 2020/2021 zilizoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
“Mheshimiwa Rais Samia anawahakikishia kuwa Serikali anayoiongoza imedhamiria kuendeleza michezo na itaongeza nguvu ili kuhakikisha mchezo wa mpira wa miguu nchini unakuwa na viwango bora.”
Waziri Mkuu aliupongeza uongozi wa TFF kwa kuandaa wa tuzo hizo ambazo zinatoa motisha kwa wachezaji, walimu, viongozi wa vilabu na waamuzi. “Tuzo hizi zinaongeza hamasa kwa wengine kushiriki kikamilifu.”
“…Katika vipindi vyote, sasa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania limetufikisha mahali ambapo tunaona muelekeo wa soka letu. Viongozi wa TFF wametufikisha mahali pazuri, tunapaswa kuwapongeza kwa hatua hii.”
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa alimuagiza Mkurugenzi wa Michezo nchini Yusuph Singo ahakikishe timu zinazoliwakilisha Taifa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa zinawezeshwa kushiriki kikamilifu bila ya kukwama.
Katika hafla hiyo, Mheshimiwa Majaliwa alitoa tuzo kwa timu na wachezaji waliofanya vizuri katika makundi mbalimbali. Baadhi ya tuzo zilizotolewa ni na ya mchezaji bora VPL 2020/ 2021 ambaye ni John Bocco kutoka klabu ya Simba; Mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho, Feisal Salum kutoka Yanga Sports Club, mchezaji bora anayechipukia ambayo iliyochukuliwa na Abdul Sopu wa Coastal Union na tuzo ya mhamasishaji bora iliyochukuliwa na Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo.
Tuzo nyingine ni ya timu yenye nidhamu iliyochukuliwa na Timu ya Coastal Unioan, tuzo ya heshima kwa soka la wanawake iliyopokelewa na Mjane wa marehemu, Dkt. Maneno Tamba
Rais wa Shirikisho la Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia alimkabidhi Waziri Mkuu tuzo ya heshima kutokana na mchango wake mkubwa katika kuendeleza mpira wa miguu nchini. Pia Waziri Mkuu alimkabidhi Alhaji Abdallah Kibadeni tuzo ya mchezaji gwiji
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hizo Alhaji Ahmed Msafiri amesema kuwa utoaji wa tuzo hizo umezingatia haki na usawa kutoka kwa majaji na pia zimetolewa kulingana na vigezo vilivyowekwa ikiwemo ushiriki wa kila mmoja katika eneo husika.