*Atangaza timu za mikoa za kusimamia fedha hiyo
*Asisitiza hakuna kulipana posho, ahimiza tathmini zifanyike kila mara
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Wakuu wa Mikoa yote nchini wanapaswa kusimamia kwa karibu fedha maalum ya sh. trilioni 1.3 zilitolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ili kuimarisha huduma za jamii.
“Kule mikoani kutakuwa na kamati maalum na Mkuu wa Mkoa ndiye atakuwa Mwenyekiti wake na Katibu Tawala atakuwa Katibu wao. Pia kutakuwa na mchumi, Mhandisi wa Mkoa, Afisa Manunuzi, Afisa Elimu, Mganga Mkuu wa mkoa, Mwanasheria, Mratibu wa Sekta na tumemuongeza Mhandisi wa TARURA kwani atahitajika japo hayumo kwenye sekretarieti ya mkoa,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Alhamisi, Oktoba 21, 2021) ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma wakati alipokutana Mawaziri na Makatibu Wakuu ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kitaifa inayosimamia miradi ya fedha za kuimarisha huduma za jamii.
Waziri Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, amesema Kamati za Ulinzi za Mikoa (KUU) zitakuwa na jukumu la kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo na kama kutakuwa suala rushwa wataingia na kuchukua hatua. “Katika kipindi cha miezi tisa, tunatakiwa tuwe tumekamilisha hii miradi,” amesisitiza.
Amesema timu hiyo ndiyo itawajibika kwenda maeneo ya vijijini kuona kama kazi inafanyika kwa viwango vinavyotakiwa kwani kuna baadhi ya miradi utekelezaji wake unapaswa uwe umekamilika ndani ya miezi mitatu.
“Mkoa utaamua ni mfumo gani utumike kusimamia utekelezaji miradi kwenye wilaya zake. Waheshimiwa Mawaziri lazima mwende kukagua miradi hii kulingana sekta zenu na mkifika mkoani ni lazima muambatane na Afisa mhusika kutoka mkoani,” amesema.
Amesema Makatibu Wakuu pia wanapaswa kwenda kuangalia utekelezaji wa miradi hiyo lakini kwa kupeana zamu na Mawaziri wao. “Hii ndiyo Kamati inayosimamia hizi fedha, kwa hiyo tunatakiwa tusimamie miradi yote ya kisekta ili ikamilike ndani ya miezi tisa kama ilivyopangwa. Mheshimiwa Rais ameshasema, sisi kazi yetu ni kuhakikisha kwamba inakamilika. Tusipokwenda hakuna ambaye atawajibika.”
Waziri Mkuu amesema watendaji wa vijiji na kata nao wana wajibu wa kusimamia miradi hiyo huko huko waliko na kusisitiza kuwa wahandisi wahakikishe viwango vya majengo vinaendana na fedha zilizotolewa. Amesema mafundi wanaoajiriwa wapewe mikataba ili wasikimbie kazi.
Kuhusu manunuzi ya vifaa vitakavyotumika kwenye miradi hiyo, Waziri Mkuu amewataka wahakikishe wanatumia ledger. “Manunuzi haya si ya kutoa fedha mfukoni yakaishia hapo. Ni lazima kuwe na ledger. Nimebaini kwenye miradi mingi, BOQ zinaandaliwa lakini kwenye manunuzi, bei inakuwa tofauti na miradi inakwama kukamilika.”
“Kwenye miradi hii, wakinunua vifaa kuwe na daftari la makabidhiano baina ya mnunuzi na Kamati ya Usimamizi. Vifaa vikishanunuliwa ni lazima vikabidhiwe kwa Kamati,” amesisitiza.
Kuhusu posho, Waziri Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa amesema: “Hakuna mtu anayepaswa kudai posho katika hii kazi. Tukifanya hivyo, hii miradi haitakamilika. Hata sisi hapa kwenye Kamati hii, Mheshimiwa Rais hajatoa posho, sana sana ametuongezea majukumu,” amesisitiza.
Mapema, akiwasilisha mchanganuo wa sh. trilioni 1.3 zilitolewa na IMF, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba alisema fedha hizo zimetolewa kulingana na sekta. Sekta hizo ni maji, afya, elimu, utalii, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na hifadhi ya jamii (social protection) ambako kuna TASAF, vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
“Sekta ya maji imepangiwa sh. bilioni 139.4, afya (sh. bilioni 466.9), elimu (sh. bilioni 367.6), utalii (sh. bilioni 90.2), Zanzibar (sh. bilioni 231), TASAF (sh. bilioni 5.5), vijana, wanawake na wenye ulemavu (sh. bilioni 5) na uratibu sh. bilioni 5,” alisema.
Wajumbe wanaounda Kamati hiyo ya Kitaifa ni Waziri wa Nchi, OWM – Sera Bunge na Wenye Ulemavu, Waziri wa Fedha, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Waziri wa Maji, Waziri wa Maliasili na Utalii, Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Makatibu Wakuu wa wizara hizo.