Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani(WHO) nchini Tanzania Dkt. Tigest Ketsela Mengestu akizungumza wakati wa ziara ya usimamizi shirikishi Mkoani Arusha
Timu ya usimamizi shirikishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Afya na wadau wa afya katika picha ya pamoja Mkoani Arusha kuangalia hali ya upatikanaji wa huduma za afya sambamba na mwenendo wa utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa Uviko-19.
……………………………………………………………..
Nteghenjwa Hosseah, Arusha
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani(WHO) nchini Tanzania, Dkt. Tigest Ketsela Mengestu amesema pamoja na wananchi kupata chanjo ya UVIKO-19, wanapaswa kuendelea kutumia njia zote za kujikinga za afya ya jamii dhidi ya UVIKO-19.
Dkt.Tigest ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya usimamizi shirikishi na wataalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Afya na wadau wa Afya mkoani Arusha kuangalia hali ya upatikanaji wa huduma za afya sambamba na mwenendo wa utoaji wa huduma za UVIKO-19 katika ngazi ya jamiii Na vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo utoaji chanjo ya ugonjwa huo.
“ Mbinu hizo ni zile zile ambazo tunazifahamu yaani kuvaa barakoa, kukaa mbali baina ya mtu na mtu, kuepuka mikusanyiko isiyokuwa na lazima na kutumia vipukusi ili kupunguza uwezekana wa maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO-19,” anasema Dkt. Tigest
” Kila anapopita anaona wananchi wengi hawavai barakoa hii inaleta mashaka maana hata kama umechanja lakin bado unapaswa kuchukia tahadhari ya kujikinga mwenyewe na kuwakinga uwapendao.”
Dkt. Tigest anaongeza: ” nawasihi wananchi wa Tanzania kujitokeza kuchanja ili kupunguza athari zinazoweza kutokea endapo utapata maambukizi ya UVIKO-19 na pia kuendelea kutumia njia zote za kujikinga na ugonjwa huu.”
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Sylvia Mamkwe amesema walipokea chanjo 50,000 na mpaka Oktoba 13 mwaka huu, takribani watu 47,240 walikua wamechanjwa ikiwa ni sawa na asilimia 94 ya chanjo zilizopokelewa.
” Mpaka sasa chanjo ya Janssen imekwisha na tumepokea chanjo ya Sinopharm na wameshaanza kuwachanja wananchi.” Dkt. Mamkwe