Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt. Batilda Buriani (wapi pili kutoka kulia) kitembelea mabanda mbalimbali katika viwanja vya Nane nane Ipuli yanapofanyika maonesho ya utekelezaji wa kuelekea Kilele cha Siku ya Lishe Kitaifa ambapo Kilele chake kuhitimishwa Oktoba 23, mwaka huu.
Baadhi ya washiriki wakiwa katika viwanja vya nane nane Ipuli yanapofanyika maonesho ya utekelezaji wa kuelekea Kilele cha Siku ya Lishe Kitaifa ambapo Kilele chake kuhitimishwa Oktoba 23, mwaka huu.
***************************
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt. Batilda Buriani amewataka wakazi wa mkoa wa Tabora na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Nane nane Ipuli yanapofanyika maonesho ya utekelezaji wa kuelekea Kilele cha Siku ya Lishe Kitaifa ili kupata elimu ya afya na lishe inayotolewa na wataalamu waliopo katika Viwanja hivyo.
Balozi Dkt. Buriani ametoa wito huo wakati akifungua rasmi maonesho ya Siku ya Lishe ambayo yalianza tangu tarehe 18 Oktoba, 2021 na Kilele chake kuhitimishwa Oktoba 23, 2021.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo Balozi Dkt. Buriani amesema maonesho hayo yanatoa fursa kwa wakazi wa Tabora kupata elimu sahihi ya lishe na hivyo kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Utapiamlo nchini, kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema “Lishe bora ni kinga thabiti dhidi ya magonjwa: kula mlo kamili, fanya mazoezi, kazi iendelee”
“Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa kitakuwa tarehe 23 Oktoba, 2021 ambapo tunatarajia mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe.Dkt. Dorothy Gwajima (Mb). Lakini tutaendelea kutumia fursa ya maonesho haya kutoa elimu kwa jamii jinsi ya kutayarisha mlo kamili kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya watoto, vijana, wajawazito na wanawake wanaonyesha, wazee pamoja na wagonjwa” amesema Balozi, Dkt. Buriani.
Aidha Balozi, Dkt. Buriani amesema lishe bora ina mchango mkubwa katika kufikia uchumi wa viwanda kwa sababu inazalisha nguvu kazi ya uhakika yenye afya njema kimwili na kiakili.
“Chakula tunachokula kina nafasi kubwa katika kutuwezesha kupambanua mambo kwa usahihi, na ndio maana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliamua suala hili la lishe ni lazima liwekwe katika mikakati ya nchi yetu na kuweza kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa ni Taifa lenye watu wenye afya njema na ndio maana akasaini mikataba na wakuu wa mikoa wote nchini ambapo na mimi leo hapa nitasaini na Wakuu wa Wilaya” Amesema Balozi, Dkt. Buriani
Siku ya Lishe inaadhimishwa kwa mara ya pili toka kuanzishwa kwake ambapo kwa mara ya kwanza ilizinduliwa rasmi mkoani Dodoma mwaka 2020 na mwaka huu kitaifa inafanyika Mkoani Tabora ikiambatana na shughuli mbalimbali za utoaji wa elimu ya masuala ya afya na lishe.