Mwenyekiti wa Klabu ya Uchukuzi Alphonce Mwingira (aliyesimama) akiongea na wachezaji wa klabu hiyo katika moja ya kambi mkoani Morogoro.
………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
TIMU ya Uchukuzi SC wamehimizwa kufanya vyema kwenye michuano ya Shirikisho la michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI), iliyoanza leo kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Banaga Katabazi katika kikao na wachezaji takribani 70 wanaounda klabu hiyo inayoshiriki kwenye michezo mbalimbali.
Katabazi amewataka wachezaji hao kufanya vyema kwenye michuano hiyo, ili kuendeleza sifa ya ushindi kwa Sekta ya Uchukuzi.
“Kama ilivyoelezwa hapa na Mwenyekiti sisi tumezoea kupata vikombe na tunategemea kupata vikombe vingi wakati hu una viongozi wanategemea mlete vikombe kama ilivyozoeleka kumbe mnakazi kubwa naomba mjitume sana,” amesema Katabazi.
Hata hivyo amewapongeza viongozi wote wanaoiongoza timu hiyo, ambao wameweza kuleta ushindi kwenye mashindano mbalimbali.
Awali Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Alphonce Mwingira amesema klabu hiyo inaundwa na watumishi kutoka taasisi 14, ambapo amewataka kufanya vyema ili kutwaa ubingwa wa jumla kwa kuzoa ushindi wa kwanza kwenye kila mchezo.
“Ninashukuru sana kwa kufanikisha ushindi wa mara kwa mara na tutakabidhi vikombe vya michezo ya SHIMIWI na ile ya Mei Mosi kwa Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi baada ya michezo hii na tutakuwa na bonanza pia,” amesema Mwingira.
Naye Katibu Mkuu wa KLabu hiyo, Mbura Tenga aliwataka wachezaji kuishi kwa taratibu za klabu hiyo kwa kuwa na nidhamu ndani na nje ya kambi zote za klabu hiyo, bila kuiga za taasisi na wizara nyingine ili kuendeleza sifa za klabu hiyo.
Tenga ameitaja michezo ambayo klabu hiyo itashiriki kuwa ni pamoja na soka, netiboli, kuvuta Kamba, riadha, kuendesha baiskeli, draft, karata, darts na bao.
MWISHO