…………………………………………………………………..
Na Joseph Lyimo
Imeelezwa kuwa mgonjwa wa Uviko-19 anatakiwa kuuteketeza mswaki aliokuwa anautumia mara tu atakapopona ili asipate tena maambukizi mapya ya ugonjwa huo.
Mtaalam wa ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa Wizara ya Afya, Dkt Baraka Nzobo ameyasema hayo wakati akitoa elimu ya kukabiliana na janga la Uviko-19.
Dkt Nzobo amesema mgonjwa aliyepona Uviko-19 hapaswi kuutumia tena mswaki aliokuwa nao kabla ya kupona kwani atajiambukiza tena ugonjwa huo kupitia vijidudu vilivyobaki.
“Mswaki uliokuwa unautumia awali na kushikwa na Uviko-19 na kisha ukapona unatakiwa kuuacha kwa kuuteketeza na kutumia mswaki mpya ili usijiambukize upya ugonjwa huo,” amesema Dkt Nzobo.
Amesema pia ni hatari kuchangia dawa moja ya meno kwa familia nzima kupitia miswaki tofauti au watu wengi kutumia dawa moja ya meno mfano kwenye kambi ya wazee au shuleni.
“Mnaposhirikiana dawa ya meno kwa kupigia mswaki na kusafisha kinywa kwenye hosteli vyuoni au mikusanyiko yoyote ni hatari kwani huchangia kueneza maambukizi ya virusi vya Uviko-19,” amesema.
Dkt Nzobo amesema watu wanatakiwa kuepuka kuchangia mswaki au kuhifadhi mswaki sehemu moja ili wajikinge na maambukizi ya Uviko-19.
Mkazi wa mjini Babati Martin Gwandu amesema elimu ya Uviko-19 ni pana mno hivyo jamii inapaswa kuendelea kuelimishwa ili kuhakikisha wanaondokana na janga hilo la Uviko-19.
“Kumbe hata miswaki inaweza kuchangia maambukizi ya virusi vya Uviko-19, hilo watu wengi tulikuwa hatujalibaini kumbe tunatakiwa tuchukue tahadhari juu ya hilo,” amesema Gwandu.
Amesema elimu inapaswa kuendelea kutolewa ili jamii iweze kushiriki kukabiliana na janga la Uviko-19 kwani kuna baadhi ya mambo hawayajui ikiwemo suala hilo la mswaki.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Ally Suleiman amesema elimu hiyo ya miswaki kwenye mapambano ya Uviko-19 ndiyo ameisikia ila atachukua tahadhari pindi akitumia dawa ya meno.
“Mimi nilikuwa nimezoea kuchukua tahadhari kwa kuvaa barakoa, kuepuka mikusanyiko, kunawa maji tiritika na kutumia vitakasa mikono, suala la kuchangia dawa ya meno kwenye mswaki kumbe ni tatizo nilikuwa sijabaini hilo,” amesema.
Amewaomba wataalam wa afya waendelee kutoa elimu ya jangwa la Uviko-19 kwani hivi sasa jamii ina mwamko mkubwa wa kuwasikiliza wao ndiyo maana wanashiriki chanjo.
Kwa mujibu wa Wizaara ya Afya, hadi kufikia Oktoba 2 mwaka huu, watanzania waliothibitika kuwa na maambukizi ya Uviko-19 ni watu 26,034, vifo vilivyotokea ni 724 na waliopatiwa chanjo ni 885,579.