Meneja wa shirika la posta Mkoa wa Arusha na Manyara ,Athman Msilikale akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa wadau wa Tehama unaoendelea mkoani Arusha,(Happy Lazaro).
******************************
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Shirika la posta Tanzania ,mkoani Arusha limewataka wananchi kutumia huduma za kidigitali kupitia Tehama zinazotolewa na shirika hilo ambalo limerahisisha utoaji wa huduma zake kuwa wa kisasa na haraka zaidi.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Posta mkoa wa Arusha na Manyara,Athman Msilikale wakati akizungumza katika mkutano wa tano wa wadau wa Tehama unaoendelea mkoani Arusha.
Amesema kuwa, wao kama wadau wa Tehama wamefikia hatua ya kushiriki katika mkutano huo kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi ili wajue huduma mpya wanazotoa kutoka mfumo wa zamani wa analogi na kutumia mfumo mpya wa kidigitali ambao unamwezesha mtumiaji kuweza kupata huduma kwa haraka na kwa wakati .
Hata hivyo amewataka wananchi mbalimbali kutembelea katika banda lao lililopo katika mkutano huo ili waweze kupata elimu ya kutosha kuhusu huduma zinazotolewa na shirika hilo na hatimaye kuweza kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo.
Msilikale amesema kuwa, hivi sasa shirika hilo limebadilisha utoaji huduma zake kutoka analojia kwenda kidigitali kupitia Tehama ambapo mifumo hiyo ya kidigitali inawarahisishia wateja kuweza kupata huduma kwa haraka .
Msilikale ameongeza kuwa,shirika hilo limeweza kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo ya biashara mtandaoni,huduma za kiganjani,huduma za Posta mlangoni,huduma za EMS ,huduma za barua za kawaida na huduma ya wateja wakiwa na bidhaa zao,pamoja na huduma za Posta Cargo ambapo huduma zote hizo zinawasaidia wateja kupata huduma kwa haraka na popote pale walipo.
“Kwa hiyo tumefikia hatua ya kutumia mifumo ya Tehama na wananchi wameweza kuelewa vizuri mifumo hii hasa katika soko na kuweza kutangaza bidhaa zetu kwa njia ya mtandao na hatimaye kuweza kukuza soko la ajira ndani na nje ya nchi”amesema Msilikale.
Amefafanua kuwa,shirika hilo limeweza kuboresha huduma zake kwa kutoa huduma kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa hali ambayo imewezesha Serikali kuendelea kupata kodi.
Hata hivyo alitoa wito kwa wadau ,wananchi , Taasisi pamoja na wafanyabiashara mbalimbali kuhakikisha wanalitumia shirika hilo katika kupata huduma mbalimbali kwa kutumia mifumo ya Tehama ambayo imeboreshwa zaidi.
Mwisho