Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Sheikh Abubakar Zuberi Bin Ally, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania wakati alipowasili katika viwanja vya Kaitaba, Bukoba mkoani Kageta, wakati alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye Baraza la Maulid Kitaifa. Oktoba 19, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia kwenye Baraza la Maulidi Kitaifa, lililofanyika Kitaifa katika viwanja vya Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera. Oktoba 19, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi Bin Ally akizungumza na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu kwenye Baraza la Maulidi lililfanyika katika viwanja vya Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera. Oktoba 19, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwahutubia baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu kwenye Baraza la Maulidi lililfanyika katika viwanja vya Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera. Oktoba 19, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeonesha kwa vitendo kuongoza Taifa na kufikisha maendeleo kwa Watanzania wote bila kujali tofauti za kidini na ukabila.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imeendelea kusimamia mshikamano, haki na umoja wa Taifa, hivyo amewasihi Watanzania wote waendelee kumuombea Rais Samia ili aendelee kuiongoza vyema nchi yetu.
Ameyasema hayo leo Jumanne (Oktoba 19, 2021) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia katika Baraza la Maulid lililofanyika Kitaifa katika uwanja vya Kaitaba mjini Bukoba Mkoani Kagera.
Waziri Mkuu amewataka waumini wa dini ya Kiislam nchini watumie maadhimisho hayo kama fursa muhimu kwao kuyasoma na kuyatafsiri kivitendo maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W) katika mfumo wao wa maisha ya kila siku.
“ Tafakuri hiyo ituwezeshe kuishi maisha ya undugu, kupendana, kuheshimiana na kushikamana miongoni mwetu Waislam pamoja na Watanzania wote kwa ujumla.”
Akizungumzia suala la amani na utulivu Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa amani ni tunu adhimu ambayo Mwenyezi Mungu ametukirimia kwani kuishi kwa amani ni kumfanya ibada Mwenyezi Mungu.
“Kudumisha amani iwe ni wajibu wa kila mmoja wetu kwani amani ndiyo kila kitu. Bila amani hatuwezi kupata maendeleo, hatuwezi kufanya ibada, watoto wetu hawawezi kwenda shule na mambo mengine mengi”.
Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa kinara katika kuenzi na kudumisha amani, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuendelea kuitunza amani hiyo kwa kuwafundisha vijana na watoto misingi ya amani ili nao waidumishe.
“Serikali inatambua umuhimu wa madhehebu ya dini katika kudumisha amani. Viongozi wa dini mmekuwa mabalozi wema na kudumisha amani yetu kwa miongo kadhaa. Jitihada zenu zote zimewezesha nchi yetu kupata utulivu kila wakati na aghalabu kuwa kimbilio la majirani pindi wanapopata machafuko.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwasihi viongozi wa dini kuwaelimisha waumini wao kufanya maandalizi kwa ajili ya kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi ambayo inatarajiwa kufanyika Agosti mwakani.
“Zoezi hili litaiwezesha nchi kupata takwimu za msingi zinazotumika katika kutunga sera, kupanga mipango na programu za maendeleo pamoja na kufuatilia utekelezaji wake.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kuchanja chanjo ya kujikinga na UVIKO 19. “Suala la afya ni muhimu na si la kufanyia maskhara.Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Samia ameshazindua kampeni ya chanjo dhidi ya UVIKO 19. Tumuunge mkono.”
Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally amewasihi wananchi waendelee kuwaheshimu na kuwatii viongozi wao wa dini na Serikali kwa sababu hiyo ndiyo tabia njema ambayo inachangia Taifa kuwa na maendeleo.
Naye, Katibu Mkuu wa BAKWATA, Sheikh Nuhu Jabir ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia kwa namna inavyowahudumia wananchi kwa kutoa takribani trilioni moja kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.