………………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MKUU Wa Wilaya ya Kibaha ,Mkoani Pwani, Sara Msafiri amemuagiza ofisa mazingira,biashara na afya kusimamia agizo la kuwaondoa wafanyabiashara wa eneo la Pichandege na kuhakikisha wanahamia Msufini River Road kupisha upanuzi wa barabara.
Aidha amepiga marufuku wenye maduka kuuza bidhaa za sokoni na mbogamboga na kuwaasa kulinda miundombinu ya barabara iwe safi.
Ameeleza ni mara ya nne uongozi wa wilaya umekwenda kuongea na kutoa onyo kwa wafanyabiashara hao lakini wanaonekana kukaidi agizo la serikali.
Msafiri aliyaeleza hayo ,wakati alipofika kwa mara ya mwisho eneo hilo na kutoa amri ya kuondolewa kwa nguvu oktoba 19 mwaka huu ili kuacha eneo hilo wazi.
Alisema , wafanyabiashara baadhi yao wamekuwa wakipenda kuhamishwa kwa nguvu badala ya kutii kwa hiari Jambo ambalo sio zuri.
Alisema mwisho ilikuwa tarehe moja Oktoba mwaka huu ,ambapo ni muda wa kutosha .
“Shirika la elimu limeshatoa eneo na miundombinu yote ya maji,umeme ,barabara,vyoo vipo ,sasa tumekuja kuwaondoa wote ,
“Kama una bidhaa za sokoni nendeni sokoni ,huwezi ukawa na leseni ya maduka ukauza mchicha mbogamboga,matunda,nyanya mbele ya duka lako ,Ni ukiukwaji wa leseni yako uliyopewa,'”;! maeneo ya kutosha yameshatengwa ,limeongezwa na eneo la mnada ,hivyo Ni makosa kufanya biashara maeneo yasiyo rasmi”:alifafanua Msafiri.
Msafiri alieleza kwamba ,maeneo ya Pichandege yaachwe wazi ,na ihakikishwe yanakuwa safi .
Nae Ofisa Mazingira Mji wa Kibaha ,Mkana Mkana alisema kwa mujibu wa sheria ndogo ya mazingira Kibaha mwaka 2012 vipengele vyote hadi 32 inamtaka mwananchi afanye usafi maeneo ya biashara yake na kutofanya biashara nyingine nje ya leseni yake .
Mkana alieleza ,endapo mtu akienda kinyume na takwa hilo ,atakuwa ametena kosa kifungu 33 hivyo basi atatakiwa kulipa faini 50,000 ama kifungo cha miezi sita au vyote .
“Wanakiuka taratibu hivyo sheria kali ya kifungo cha miezi sita ama faini 50,000 itatolewa ama vyote kwa pamoja,Na wafanyabiashara hawa walishapewa taarifa na onyo mara kadhaa lakini bado wanakiuka.”alisisitiza Mkana.
Ofisa biashara Mji wa Kibaha, Adolf Msangi, alibainisha wafanyabiashara hao wanapaswa waondoke na pia maeneo bado yapo kama wapo ambao hawataki kuhamia Msufini basi waende loliondo Kama sio loliondo waende Lulanzi .
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa wafanyabiashara, Daniel singa alisema maeneo yapo ya wafanyabiashara wote waende wakagawiwe maeneo na kuacha kukaidi.