Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Ujenzi wa jengo jipya la Ofisi ya Waziri Mkuu katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma Tarehe 18 Oktoba, 2021.Kulia kwake ni Naibu Waziri wake (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi na kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Tixon Nzunda.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa jengo jipya la Ofisi ya Waziri Mkuu katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma Tarehe 18 Oktoba, 2021 wakati wa kikao cha uzinduzi huo kilicho jumuisha timu ya menejimenti ya ofisi yake, wakandarasi wa ujenzi na washauri elekezi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akichapia tofali kuashiria kuanza rasmi kwa ujenzi wa Majengo ya Ofisi yake katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma
Mtaalam mwelekezi kutoka Chuo Kikuu Kishiriki Ardhi Dkt. Godwin Maro akiwasilisha michoro ya mwonekano wa majengo mapya ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) yanayotarajiwa kujengwa eneo la Mji wa Serikali Dodoma.
Baadhi ya Timu ya Menejimenti Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo anayeshughulilia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi huo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Tixon Nzunda akifafanua jambo wakati wa kikao hicho..
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akichanganya mchanga kuashiria kuanza rasmi kwa ujenzi wa majengo ya ofisi hiyo katika eneo la Mji wa Serikali Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama pamoja na Naibu Waziri wake Mhe. Patrobas Katambi (wa tano kutoka kulia), Katibu Mkuu Ofisi hiyo, Tixon Nzunda (kushoto kwa waziri) na Manaibu Katibu Wakuu Prof. Jamal Katundu (wa tatu kutoka kulia), na Kaspar Mmuya (wanne kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wakandarasi kutoka SUMA JKT, washauri elekezi kutoka Chuo Kikuu Kishiriki Ardhi pamoja ma
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
……………………………………………………………………..
Na: Mwandishi Wetu – Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema Rais wa Awamu ya Sita Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametenga shilingi bilioni 6 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi za serikali awamu ya pili ili majengo hayo yaanze kutumika kwa haraka.
Ameyasema hayo hii leo Oktoba 18, 2021 wakati wa hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa majengo mapya ya Ofisi ya Waziri Mkuu awamu ya pili katika Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.
Waziri Mhagama alisema kuwa, toka Serikali ilipotangaza azma ya kuhamishia shughuli zake Makao Makuu ya nchi, mwezi Septemba, 2016, hadi kufikia Juni, 2021 jumla ya Watumishi 18,300 wamekwisha hamia Jijini Dodoma na katika kipindi hicho shilingi bilioni 655, 886, 878, 308.83 zilitumika kuhamisha watumishi pamoja na kuwezesha ujenzi wa majengo ya Ofisi za Awali za awamu ya kwanza na miundombinu muhimu katika Wizara 23.
“Nitumie fursa hii kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuendeleza nia na maamuzi ya Serikali kuhamia Jijini Dodoma kwa vitendo pamoja na kuridhia mpango mkakati wa ujenzi wa majengo ya ofisi za Serikali awamu ya pili,” alisema Waziri Mhagama
Alifafanua kuwa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameridhia jumla ya shilingi bilioni 600, 884, 941, 784.70 katika kuhakikisha awamu ya pili ya ujenzi wa mji wa Serikali yanakamilika.
“Katika mwaka wa fedha 2021/2022 shilingi bilioni 300 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo ya serikali,” alisema
Aliongeza kuwa, ujenzi wa majengo katika mji wa Serikali awamu ya pili yatakuwa na muundo wa ghorofa na kila jengo litakuwa na ghorofa 6 kwenda juu na hapatakuwa na jengo lenye idadi ndogo ya ghorofa hizo.
“Kipekee Ofisi ya Waziri Mkuu tunampongeza Mhe. Rais kwa kupata fursa ya kujenga majengo mawili kupitia ujenzi huu wa majengo haya ya Serikali katika awamu hii ya pili,” alisema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito kwa Wizara zote kukamilisha kwa haraka utaratibu wa kupata wakandarasi kama ilivyoagizwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mikataba yote ya ujenzi ihakikishwe inazingatia thamani ya fedha na viwango katika ujenzi unaotarajiwa kuanza, Taasisi zinazohusika na huduma na miundombinu zihusishwe katika ujenzi na utekelezaji wa Mradi Taasisi ikiwemo, DUWASA, TANESCO, TTCL, Zimamoto, NEMC, OSHA, TFS na GSO na pia amezitaka kamati za ndani za ufuatiliaji na usimamizi kuhakikisha wanatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi na changamoto zinazojitokeza ili kuzipatia ufumbuzi.
Aidha, Waziri alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi wa jiji la Dodoma kuchangamikia fursa mbalimbali wakati wa ujenzi wa majengo hayo ya Serikali katika awamu hii ya pili.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Tixon Nzunda aliahidi kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa Waziri huku akimuhakikishia kusimamia mradi huo kwa viwango vinavyo hitajika na kukabidhi mradi huo kwa wakati.
“tumesha saini mkataba na kumaliza taratibu za manunuzi na kukabidhi rasmi kazi za kuanza ujenzi, na hadi sasa kazi za awali zinaendelea ikiwemo kusafisha eneo la mradi. Miradi hii itatekelezwa kwa kipindi cha miezi kumi na sita badala ya ishirini na nne kama ilivyokuwa awali,” alisema Nzunda