Chifu Kingalu Mwanabanzi 15
Wazee walioshiriki Tambiko wakiimba.
Hao ni baadhi ya wanafamilia wa machifu waliotangulia wakitambulishwa katika tambiko hilo.
Sanamu ya kuchongwa na mti ikionesha namna Chifu Kingalu wa kwanza alivyokuwa..
……………………………………………………………………
Adeladius Makwega,KINOLE –WUSM
Chifu KIngalu Mwanabanzi 15 amekamilisha tambiko la kabila la Waluguru ambalo limedumu kwa siku mbili huku akiomba viongozi wa Serikali kuendelea kushiriki katika shuguli mbalimbali za kichifu ili kuombea mambo kadha wa kadha kwa maendeleo ya taifa la Tanzania akisema kuwa Chifu Kingalu ni miongoni mwa machifu nane walikuwa wanasimamia majimbo hayo wakati wa Uhuru wa Tanganyika ambao walimuunga mkono Mwalimu Julius Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa kudai Uhuru wa Tanganyika.
Kauli hiyo ya kiongozi huyu wa kimila imetolewa Oktoba 17, 2021 katika sherehe hiyo iliyodumu kwa siku kadhaa ikiwakutanisha watu mbalimbali katika tambiko linalofanyika mara moja kila mwaka katika makazi ya Chifu Kingalu yaliyopo katika kjiji cha Kinole kilomita kadhaa kutoka Mji wa Morogoro.
“Mheshimiwa Jakaya Kikwete Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifika na kukutana na mtangulizi wangu Chifu Kingalumwana Banzi wa 14 na mambo kadhaa yalifanyika na hata yeye kuweza kuongoza vizuri sana bila ya kupata matatizo makubwa na hata hapo awali Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kufika na kula ugali na mboga za asili hapa hapa Kinole. ”
Alibainisha kuwa mara chache sana kwa Chifu kusema maneno kama haya lakini anafanya hivyo akiwa na maelekezo ya wazee ili kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele kwa amani na utulivu.
“Kwa sasa kuna changamoto za ugonjwa wa Korona kwa hakika tayari tumeshaliombea huku tukimuombea pia Rais Samia Suluhu ili aweze kuvuka katika suala hili kwani kwa sasa zipo pande zinazosigishana juu ya chanjo ya ugonjwa huo.Tumeombea mvua inyeshe kulingana na mahitaji ya jamii, vijana wa Kitanzania wawe na maadili mema na pia amani na utulivu ya taifa letu iendelee kutamalaki.”
“Ninaomba serikali iwekeze katika maeneo ya machifu nchini kwani kwa sasa gharama za kuyatunza na kuyahifadhi ni kubwa sana kwa hiyo machifu wengi tunashindwa, lisipofanyika hilo maeneo haya yenye urithi wa utamaduni wetu yatapotea.”
Aidha Chifu Kingalu Mwanabanzi aliomba kuadikwa vizuri kwa jina la Soko la Morogoro Mjini ambalo lilipewa jina kwa heshima yake akidai kuwa maneno ya jina hilo yameandikwa bila ya kuweka nafasi ya kati ya neno na neno.
Nayo Serikali kwa upande wake imesema kuwa kuwa itaendelea kushirikiana katika matukio haya kwani yana umuhimu kwa mustakabali wa taifa letu kwani mila na utamaduni wa jamii umebeba uhai wa kila jamii na hizo jamii ndipo taifa huundwa.
Akizungumza katika tambiko hilo Mkurugenzi wa Idara ya Mendeleo ya Utamaduni nchini wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel Temu amesema kuwa yale yote yaliyozungumzwa na Chifu Kingalu Mwanabanzi yatafanyiwa kazi kulingana na uwezo wa serikali huku ushirikiano kati ya machifu na serikali utaendelea kudumishwa.
Dkt Temu ambaye aliambatana na maafisa kadhaa wa wizara hii amesema kuwa kwa siku zote tatu wameweza kushiriki na kujionea kwa vitendo kila kinachofanyika tangu mwanzo hadi mwisho wa tambiko.
“Ninatoa uhakisho kuwa huu ushirikiano uliopo utakuwa maradufu kwani machifu wengi ni wadau wa maendeleo wa taifa letu tangu enzi za mababu.Tuendelee kushirikiana huku tukienzi na kutunza utamaduni wetu.”
Katika tambiko hilo mambo kadhaa yalifanyika huku wasaidizi kadha wa Chifu Kingalu Mwanabanzi wa 15 wakitambulishwa na vifaa mbalimbali vya kimila vikiwamo vinyango vinavyofanana na mwanahiti, ngoma zilizowamba miaka mingi kwa ngozi za wanyama mbalimbali zilioneshwa.