Mbunge wa jimbo la Igunga wilayani Igunga mkoani Tabora Nicholaus Ngassa akizugumza na wananchi wa jimbo laken hawapo pichani
…………………………………………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
Mbunge wa jimbo la Igunga wilayani Igunga mkoani Tabora Nicholaus Ngassa amewapa siku 90 viongozi watatu akiwemo mtendaji wa kata ya Mwamashimba Michael Kasitu na mtendaji wa kijiji cha Jogohya Edward Kitenya pamoja na mwenyekiti wa kijiji cha Jogohya Joseph Thomas wawe wamekamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Jogohya ndani ya miezi mitatu.
Mbunge huyo amelazimika kutoa maagizo hayo baada ya kutembelea katika kijiji hicho cha Jogohya na kukuta ukarabati wa zahanati ukiwa haujafanyika licha ya serikali kutoa Mil. 50 za ukarabati.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona zahanati hiyo imejengwa kwa nguvu za wananchi tangu mwaka 2005 ambapo serikali imeamua kuunga nguvu za wananchi kwa kutoa Mil. 50 ili wananchi waweze kupata huduma karibu lakini uongozi umeshindwa kusimamia ukarabati wa zahanati hiyo.
“Ndugu zangu wananchi ni jambo la kusikitisha sana serikali imetoa fedha huu ni mwezi wa sita lakini hakuna kinachoendelea hivyo basi natoa siku 90 mtendaji wa kata na mtendaji wa kijiji na mwenyekiti wa kijiji hicho muwe mmekamilisha ujenzi wa zahanati na endapo mtashindwa pindi nitakaporudi januari mwakani 2022 nikikuta zahanati haijakamilika nitaagiza vyombo vya dora kuwakamata na kuwaweka mahabusu”. Alisema huku akishangiliwa na wananchi.
Hata hivyo mbunge huyo alisema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassani amekuwa akitafuta fedha kwa ajili ya kuwasaidia watanzania ikiwemo kuwasogezea huduma ya matibabu wananchi karibu lakini baadhi ya watumishi wameshindwa kutekeleza majukumu yao hivyo basi amewataka wabadilike.
Pamoja na kutoa siku 90 pia ameiandikia barua taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa wilaya ya Igunga kufanya uchunguzi wa Mil. 50 zilizopelekwa katika kijiji hicho cha Jogohya.
Nae kamanda wa Takukuru wilaya ya Igunga Francis Nzuakuu amekiri kupokea barua kutoka kwa mbunge wa Igunga Nicholaus Ngassa ikimtaka kufanya uchunguzi wa Mil. 50 katika zahanati ya kijiji cha Jogohya.
Kwa upande wake mtendaji wa kata ya Mwamashimba Michael Kasitu alisema yuko tayari kutekeleza yeye na viongozi wenzake maelekezo yaliyotolewa na mbunge wa jimbo la Igunga la kukamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho cha Jogohya.
Aidha mtendaji kata huyo alibainisha kuwa wao hawajachelewesha ukarabati wa zahanati hiyo huku akitupia lawama upande wa manunuzi katika halmashauri ya wilaya ya Igunga ambao ndio wamechelewesha kupeleka vifaa vya ujenzi.
Sambamba na hayo alisema fedha hizo Mil. 50 ni nyingi sana ambapo wangekabidhiwa uongozi wa kata ya Mwamashimba wangeweza kujenga na nyumba ya mtumishi mmoja wa afya.
Mwenyekiti wa kijiji cha Jogohya Joseph Thomas alisema atahakikisha anasimamia ukarabati wa zahanati hiyo usiku na mchana ili zahanati ikamilike ndani ya siku 90 walizopewa na Mbunge.
Kwa upande wake mkandarasi aliyepewa tenda ya kukarabati zahanati hiyo Daudi Masaga Kibe alisema angekuwa ameishamaliza siku nyingi ukarabati lakini kila anapofuatilia vifaa vya ujenzi katika idara ya manunuzi amekuwa akipigwa danadana na kusema kuwa amemshukuru Mbunge kusimamia suala hilo huku akisema kuwa walikubaliana ujenzi kwa gharama ya Mil. 8.