…………………………………………………….
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Doto James akiwa Dubai amefanya kikao kwa njia ya mtandao (zoom) na baadhi ya Wakurugenzi wa Taasisi za Serikali ili kuchochea msukumo wa ushiriki wa uhakika wa Taasisi za Serikali kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai.
Kikao hiki pia kilihudhuriwa na Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai Balozi Mohammed Abdallah Mtonga na Mkuu wa Banda Bi.Getrude Ng’weshemi.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Taasisi walioshiriki ni Mkurugenzi wa Shirika la Reli (TRC) Bw. Masanja Kadogosa, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Bw. Erick Benedict Hamis, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio, Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha J. Mshomba, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Bi. Bettyrita Lyimo na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar Bw. Shariff Ali Shariff (ZIPA).
Maonesho haya yalianza rasmi tarehe 01 Oktoba, 2021 yakizileta pamoja nchi 191 ulimwenguni chini ya kauli mbiu moja kubwa ya “Connecting Minds, Creating the Future” na yanategemewa kuhitimishwa mwakani tarehe 31 Machi, 2022. Tanzania imefanikiwa kuwa na banda katika maonesho haya na iliamua kushirki rasmi chini ya kaulimbiu ndogo ya ‘Mobility’ ambayo inaitangaza Tanzania na Miradi Mkubwa ya Miundombinu kupitia kauli ya ‘Connectivity, Tanzania ready for takeoff!’.
Baadhi ya miradi hiyo mikubwa ambayo imetekelezwa na mingine inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Rais. Samia Suluhu Hasaan itakayowavutia wawekezaji wakubwa sio tu kutoka Umoja wa Nchi za Kiarabu bali ulimwengu mzima. Miradi hiyo ni pamoja na Mradi Mkubwa wa Reli ya Kisasa chini ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mradi wa Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), Mradi ya maboresho ya Bandari, Mradi wa gesi asilia iliyosindikwa (LNG) na Usafiri wa Anga (ATCL).
Baadhi ya Taasisi ambazo zimetangulia kushiriki ni TANESCO ambao wanaonesha fursa ya uwekezaji kwenye Sekta ya Nishati kwenye Mradi wa Umeme wa Mto Rufiji (JNHPP) na TANAPA ambao wanaonesha fursa zilizopo kwenye Sekta ya Utalii.
Kupitia kikao hiki pia Katibu Mkuu Doto James ameendelea kusisitiza kuwa maonesho haya ni makubwa na kufuatia tamko rasmi lililotolewa kwenye Vikao vya Makatibu Wakuu chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein A. Kattanga. Amesisitiza Taasisi hizo za Serikali na binafsi kushiriki na kutumia fursa hii kuitanzanga Tanzania Duniani ili kuonesha fursa zilizopo nchini na kupata wawekezaji katika sekta mbalimbali.
Aidha, Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania Balozi Mohemmed Abdallah Mtonga ameongeza kuwa tayari waratibu wamejipanga kupokea miradi hiyo ambayo inategemea kupata wawekezaji, hivyo ni vema Taasisi zikawasilisha orodha za miradi mbalimbali ambayo inatafuta wawekezaji ili kuratibu mikutano na wawekezaji hao. Amesema, “Kwa mujibu wa taratibu zilizokuwepo, tutakuwa tunawakutanisha Taasisi hizo na wawekezaji kupitia mikutano ya Kibiashara ya mara kwa mara itakayopangwa. Kwahiyo ni vyema tukaweka utaratibu wa jinsi Taasisi zetu zitakavyo itangaza Tanzania na miradi mikubwa inahyohitaji wawekezaji”.
Hii ni nafasi ya kipekee ya miezi sita kutokea kila baada ya miaka 5. Hii ni nafasi adhimu kwa Tanzania miongoni mwa nchi nyingi duniani kushiriki katika maonesho ya Expo 2020 Dubai, hivyo watanzania walio Dubai na walio nyumbani wamehimizwa kuja kushiriki na kuunga mkono ushirikia wa Tanzania kwa nguvu zote ili fursa hii ilete faida kwa Tanzania na watanzania.