Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo. Dkt Hassan Abbasi (kushoto) leo Oktoba 18, 2021 amekabidhi rasmi Idara ya Habari MAELEZO na Sekta ya Habari kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Dkt, Zainabu Chaula (kulia) huku akipongeza uamuzi huo alioufanya Rais Samia Suluhu Hassan ambao ameuelezea kuwa ni uamuzi muhimu na wa kimkakati wa kuboresha sekta zote kwa maslahi mapana ya Taifa..
………………………………………………
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo. Dkt Hassan Abbasi leo Oktoba 18, 2021 amekabidhi rasmi Idara ya Habari MAELEZO na Sekta ya Habari kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Dkt, Zainabu Chaula huku akipongeza uamuzi huo alioufanya Rais Samia Suluhu Hassan ambao ameuelezea kuwa ni uamuzi muhimu na wa kimkakati wa kuboresha sekta zote kwa maslahi mapana ya Taifa.
Dkt. Abbasi ambaye ameilea sekta hiyo kwa miaka mitano na miezi miwili na siku 9 amesema maamuzi hayo yamekuja wakati mwafaka na kusisitiza kuwa sekta hizo zimewekwa mahali patapotakiwa na kwamba ufanisi kwenye sekta hizo utaongezeka na kuleta mafanikio makubwa tofauti na awali.
Amewataka wataalam na waandishi wa habari kote nchini kuzingatia misingi ya taaluma ya habari na kanuni kuu za maadili ambazo amezitaja kuwa ni ukweli, usahihi na umakini ili kusaidia na kuchangia maendeleo ya nchi.
“Ndugu zangu napenda kuwasihi na kuwaambia Uandishi wa Habari ni taaluma hivyo kuweni na wivu na kulinda taaluma yenu kwa kutimiza haki na wajibu wenu, ni vema mkazingatia taratibu za uandishi kuna mambo ambayo mnaruhusiwa kisheria na mambo ambayo yanakatazwa na sheria za nchi basi ni muhimu sana kuzingatia.”ameongeza Dkt. Abbasi
Aidha, ameishukuru Serikali kwa kumpa nafasi ya kutoa mchango wake kwa Sekta na Idara ya Habari na ameahidi kutoa ushirikiano wa dhati wakati wowote ambapo kwa sasa anabaki kuwa mtaalamu, mdau na wa sekta hiyo.
Akifafanua baadhi ya mambo aliyokabidhi, amesema amekabidhi ofisi ikiwa na watumishi 37, magari manne pamoja na Sheria ya Huduma za Habari na Kanuni zake ambayo ndiyo mwongozo mkuu kwenye sekta hiyo.
Kwa upande wake Katibiu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainabu Chaula amempongeza Dkt. Abbasi kwa kazi kubwa aliyofanya kwenye sekta hiyo na amemhakikishia kuendelea kufanya kazi za taaluma ya habari kwa uadilifu.
“Nikupongeze sana kaka yangu Dkt. Abbasi tumefanya kazi kwa karibu, tunategemeana tutaendelea kuboresha pale tulipoacha” ameongeza Dkt. Chaula
Akitoa shukrani kwa niaba ya Idara ya Habari- MAELEZO kwa Makatibu Wakuu hao, Mkurugenzi wa Idara hiyo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amemshukuru Mhe. Rais kwa uamuzi huo na kumpongeza Dkt. Abbasi kwa mapinduzi makubwa aliyoyafanya katika kipindi chote alichokuwa akiilea sekta hiyo.
“Niseme wazi ndugu zangu nampongeza sana Dkt. Abbasi amefanya kazi kubwa sana kwenye sekta hii na kuiheshimisha taaluma hii hapa nchini”. Amefafanua Msigwa.