………………………………………………………..
Nteghenjwa Hosseah, Arusha
Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini(TARURA) imetenga Sh bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha salam za Ofisi ya Rais-TAMISEMI wakati wa mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi wa Wilaya ya Longido tarehe 18.10.2021.
Amesema Wilaya hii imeanzishwa mwaka 2007 na kwa kipindi chote hicho haikuwahi kupata fedha za maendeleo ila kwa mwaka huu wa fedha Sh bilioni 2.2 zimetengwa kwa ajili ya maendeleo ya barabara.
“ Longido ilikuwa ikipata f fedha kidogo kwa ajili ya matengenezo na kwa mwaka jana walipata mil 835 tu lakini Mtandao wa barabara wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido ni km 695 na kati ya hizo km 1.8 ni lami, km 185 ni changarawe na udongo ni km 508”
Fedha hizo bil. 2.2 zinakwenda kutekeleza kazi ya kujenga kilomita 1 ya lami, madaraja 8 na kupandisha hadhi barabara za udongo zenye kilometa 64 kuwa changarawe.
Kuhusu sekta ya elimu, Mhe Ummy amesema Serikali pia imetenga takribani Sh bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 12 ya Sekondari na 50 katika vituo shikizi.
Alisema pia fedha hizo zitajenga maabara 10 katika shule tano za Sekondari za Natron, Katumbiine, Namanga, Lekule na Longido.
Akizungumza utekelezaji wa Mpango wa Elimu bila malipo, Mhe Ummy ameweka wazi kuwa katika kipindi miezi sita serikali imepeleka Sh bilioni 3.7 kwa ajili ya elimu bila malipo katika Wilaya ya Longido na Serikali itaendelea kuhudumia elimu bila malipo kote nchini.
Aisha, Mhe. Ummy amesikitishwa na kutokamilika kwa wakati ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Longido wakati fedha takribani Sh bilioni 1.8 zimetolewa sambamba na fedha za vituo viwili vya Afya viwili na kusisitiza kuwa wote waliohusika na uzembe huo watawajibishwa ipasavyo.