…………………………………………………………………………
Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo akutana na wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa za viwandani kujadili hali ya upatikanaji na uzalishaji wa bidhaa muhimu nchini hususan bidhaa za ujenzi kulingana na ongezeko la mahitaji.
Prof. Mkumbo amekutana nao Oktoba 15, 2021 Jijini Dar es salaam baada ya Tanzania kunufaika na fedha za mkopo wa shilingi Trilion 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani zitakazotumika kutekeleza miradi ya maendeleo itakayohitaji bidhaa za ujenzi ikiwemo kuboresha huduma za jamii katika sekta ya afya, elimu na maji.
“Tumekutana kubadilishana mawazo, kupeana taarifa na mapitio kuhusu hali ya upatikanaji wa bidhaa muhimu hapa nchini hasa bidhaa zinazohusiana na ujenzi kama mnavyojua kwa sasa sekta ya ujenzi imepamba moto hapa nchini hivyo ni muhimu tujiridhishe kama tuna bidhaa za kutosha zinazokidhi mahitaji ya ujenzi” ameeleza Prof. Kitila Mkumbo
Prof. Mkumbo ameeleza kuwa kuna malalamiko mengi mtaani kuhusu kupanda kwa bei za vifaa hususani saruji, mabati na ndondo ambapo lazima wajadili.namna ya kishuka kwa bei na kubaki katika hali ya kawaida na kudhibiti upandaji bei kiholela.
Ameeleza kuwa kupitia mkopo wa shilingi Trilion 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani zitakazotumika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo kuboresha huduma za jamii katika sekta ya afya, elimu na maji itakayohitaji bidhaa za ujenzi ambayo ni fursa kubwa,.
Ametolea mfano kutajengwa madarasa 15,000 kwa wakati mmoja nchi nzima ambayo yana hitaji bidhaa kutoka kwao kama mifuko ya saruji 2,685,000 sawa na tani 134,250 ndani ya kipindi cha miezi tisa.
Aidha, Prof. Mkumbo ameeleza kuwa Serikali imeamua kuwa wafanyabiashara, wenye viwanda na sekta binafsi kwa ujumla kufanya kazi kwa ukaribu ili kuendelea kujenga uchumi wetu maana uchumi hauwezi kujengwa na Serikali tu bila sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji.
Prof. Mkumbo ametoa wito kwa wazalishaji na wafanyabiashara kuzingatia ubora wa vifaa vinavyokwenda kwenye miradi ya Serikali vilevile kuzingatia maadili katika biashara hasa kwa baadhi ya wafanyabiashara na wazalishaji wanaoshirikiana na baadhi ya watumishi wa umma kutumia nafasi hizo kuhujumu miradi kwa njia tofauti kama kutokuzingatia ubora na kutengeneza mianya ya rushwa kwa kutokutoa risti na gharama sahihi ya bidhaa zao.