…………………………………………………………………..
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Wanafunzi ya kidato cha nne katika shule ya St.Francis iliyopo Manispaa ya Shinyanga wameaswa kutojihusisha na vikundi vya vishawishi vinavyoweza kupelekea kuteteleka kimaadili miongoni mwao.
Hayo yamesemwa na mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Mkurugenzi wa Empire Hotel iliyopo mkoani Shinyanga Dk. Ernest Haraka kwenye mahafali ya kidato cha nne ya shule hiyo ambayo yamefanyika leo kwenye viwanja vya shule hiyo.
Dk. Ernest amebainisha kuwa mtaani kuna vikundi mbalimbali vya ushawishi hivyo amewataka wanafunzi hao pinsi watakapohitimu kuhakikisha wanajiepusha navyo ili kujilinda kimaadili kwa ustawi wa maisha yao.
“Kuna kazi moja iko mbele yenu ambayo ni kazi ya kurudi kwa wazazi kwa muda na badaye kwenda kule sasa isitokee wengine mkaanze kubadirisha taratibu zenu za maisha nawaombeni sana ninyi wahitimu mkienda nyumbani kunamagenge mabaya yapo na kubadilika ni sekunde tu unakuwa ni mtu mwingine kabisa naomba kitu hicho mkiepuke nitashukuru kama sitosikia kwamba mwanafunzi wa St. Francis amekutwa mtaani anazunguka zunguka lakini hata sisi wazazi mtambue kuwa hawa bado wanaakili ambayo inakuwa sasa muwe tayari kuwasaidia, kuwasikiliza na kuwakanya”
Sherehe ya mahafali hayo imetanguliwa na ibada ya Misa takatifu iliyoongozwa na Paroko wa kanisa kuu la Mama Mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Mjini Shinyanga Padre Adolf Makandagu ambaye amewataka wanafunzi hao kudumu katika imani kwa Mungu katika safari ya kuelekea kufanya mtihani wa taifa wa kuhitimu kidato cha nne.
Padre Makandagu amesema kuwa Mungu pekee ndiyo amekuwa kiongozi kwa kuwawezesha wanafunzi hao kufikia hatua hiyo hivyo wanahitaji kuendelea kumuamini ili aweze kuwawezesha pia kufaulu mitihani yao
“Tulisikia shule ya St.Francis lakini imani ilitutuma hapa kwamba tukienda pale tutafikia malengo yetu ya maisha kama kweli imani hiyo mtaendelea kuwa nayo mtihani unaokuja mtashinda, leo hii mnashukuru Mungu lakini mnaamini kwa imani yenu mliyonayo mtapiga hatua kikubwa naomba muwe na imani kwa Mungu atawasaidia kufaulu mtihani”
Kwa upande wake Meneja wa shule ya St. Francis Paulo Mahona amewaasa wanafunzi wahitimu kwenda kuyazingatia yale yote waliyofundishwa ya kitaaluma, kiroho na kimaadili kwa kutambua kuwa bado ni wanafunzi ambapo amewataka kutokukata tamaa katika safari ya maisha kupitia elimu huku akiwasisitiza kutamani kupata elimu ya juu zaidi
Sherehe ya Mahafali ya 7 kidato cha nne ya shule ya sekondari St. Francis yamefanyika kwenye viwanja vya shule hiyo