Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Mwanza katika utaratibu wake wa kila wiki wa kutoa taarifa za utendaji kazi za Serikali.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akionesha Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Mwanza, picha rasmi yenye alama muhimu (QR code) ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan inayotakiwa kutumika kwenye ofisi na maeneo mbalimbali.
Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC), Abubakar Karsan akiuliza swali katika mkutano kati ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa na Waandishi wa Habari leo jijini Mwanza.
Waandishi wa habari wakiuliza maswali wakati Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Mwanza katika utaratibu wake wa kila wiki wa kutoa taarifa za utendaji kazi za Serikali.
Baadhi ya waandishi wa habari wakipokea vyeti ikiwa ni pongezi kutoka Klabu ya Waandishi wa Mkoa wa Mwanza, baada ya kushinda Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) kwa mwaka 2020.
(Picha zote na Immaculate Makilika- Idara ya Habari-MAELEZO, Mwanza)
…………………………………………………………………………………………….
Na Ahmed Sagaff – MAELEZO
Mkoa wa Mwanza umepokea shilingi Bilioni 344 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya wananchi katika kipindi cha miezi sita ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hayo yameelezwa leo jijini Mwanza na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alipokuwa akitoa taarifa ya kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Amesema kiasi hicho cha fedha kimeelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi (bilioni 219.1), sekta ya afya (bilioni 15.2), sekta ya elimu (bilioni 38.7), miundombinu ya barabara (bilioni 2.4), usambazaji wa umeme vijijini (bilioni 42.6), miradi ya maji (bilioni 20.4) na mradi wa kusaidia kaya masikini unaotekelezwa na TASAF (bilioni 5.6).
Pamoja na hilo, Msigwa amehabarisha kuwa fedha hizo zitaendeleza ujenzi wa Stendi za Nyamhongolo na Nyegezi, Soko la Kisasa la Mjini, Jengo la Abiria pale kwenye uwanja wa Ndege wa Mwanza, ujenzi wa MV Mwanza yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo, na Daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2.
“Tumeleta shilingi Bilioni 8.3 kwa ajili ya kujenga hospitali tatu za Wilaya ya Sengerema, Kwimba na Misungwi, kumalizia hospitali mbili za Wilaya ya Buchosa na Ilemela, kujenga vituo vya afya vitano na zahanati 21 na kukarabati na kujenga vituo vya huduma 48, aidha tumeleta shilingi Bilioni 6.4 kwa ajili ya kununua dawa,” amefahamisha Msigwa.
Akifafanua kuhusu shilingi bilioni 38.7 zilizoelekezwa kwenye sekta ya elimu mkoani Mwanza, Msigwa ameeleza kuwa shilingi bilioni 11 zinaimarisha miundombinu ya elimu kwenye shule za msingi na sekondari huku shilingi bilioni nane zikigharamia mradi wa elimu bila malipo.
“Na tunatarajia kuleta shilingi bilioni 19.7 kwa ajili ya kujenga madarasa 985, hizi ni zile fedha za Mpango wa Ustawi wa Jamii tulizopata kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF),” amedokeza Msemaji Mkuu wa Serikali.
WATANZANIA 7,713 WAAJIRIWA MRADI WA BWAWA LA UMEME RUFIJI
Na Ahmed Sagaff – MAELEZO
Watanzania 7,713 wanafanya kazi kwenye Mradi wa Bwawa la Kufulia Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) unaotekelezwa wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ameyasema hay oleo jijini Mwanza alipokuwa akieleza kazi zinazofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Wafanyakazi 7,713 ambao ni sawa na asilimia 89 ya wafanyakazi wote 8,635 waliopo katika mradi huu ni Watanzania,” ameeleza Msigwa.
Sambamba na hilo, amefahamisha kuwa wakandarasi wanaotekeleza mradi huu wameshalipwa shilingi trilioni 2.832 ambayo ni sawa na asilimia 35.62 ya fedha zote shilingi trilioni sita na bilioni 558 zitakazotumika kugharimia ujenzi huu.
“Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango yeye wiki hii amefanya ziara katika mradi wa ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere katika mto Rufiji na kujionea kazi kubwa inayofanywa katika mradi huu,” amedokeza Msigwa.
Pamoja na hayo, Msemaji huyo amehabarisha kwamba mradi huu umebuniwa na kusanifiwa na Watanzania, na kwamba unasimamiwa na wahandisi wa Tanzania kupitia kitengo kilicho chini ya TANROADS kiitwacho TECU na unatekelezwa kwa fedha za Watanzania.
“Malighafi zinazotumika hususan tani 850,000 za saruji, tani 70,000 za nondo, tani 250,000 za pozzolana na malighafi nyingine zinatoka hapa hapa nchini kwetu,” amebainisha Msigwa.
SERIKALI YAANIKA MBINU ZA KURAHISISHA ULIPAJI MAFAO KWA WASTAAFU
Na Ahmed Sagaff – MAELEZO
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) imeandaa mbinu kabambe utakaowasaidia wastaafu kupata malipo yao kwa wakati.
Akizungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari jijini Mwanza leo, Msigwa amezitaja mbinu hizo kuwa ni ‘Data Cleanup’ na ‘Lipa Jana’.
“Na sasa PSSSF inakwenda kwa kauli mbiu isemayo “Lipa Jana” yaani wanataka mtu ukistaafu leo mafao yako yawe tayari yameshaingia kwenye akaunti yako tangu jana,” ameeleza Msigwa.
Akiifafanua mbinu iitwayo ‘Data Cleanup’, Msigwa amefahamisha kwamba ubunifu huu utaiwezesha PSSSF kuweka sawa taarifa za wafanyakazi kabla ya tarehe ya mwisho ya kustaafu.
“Lengo mtu anapostaafu kusiwe na mambo hayajakaa sawa katika taarifa zake za utumishi,” amebainisha Msigwa.
WATANZANIA 940,507 WAPOKEA CHANJO YA JANSEN
Na Ahmed Sagaff – MAELEZO
Watanzania 940,507 wamepokea chanjo ya Jansen ikiwa ni asilimia 88.9 ya chanjo zote 1,058,400 za aina hiyo zillizotolewa na Serikali ya Marekani kupitia mpango wa COVAX FACILITY.
Hayo yamesemwa leo jijini Mwanza na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alipokuwa akitoa taarifa ya kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Shehena ya chanjo 1,065,000 aina ya Sinopharm zilizokuja wiki iliyopita kutoka China zimeanza kusambazwa katika Halmashauri na Mikoa yote nchini na zoezi la uchanjaji linaendelea,” amefahamisha Msigwa.
Pamoja na hilo, amehabarisha kuwa Tanzania inatarajia kupokea chanjo zingine aina ya Pfizer dozi 500,000 mwishoni mwa mwezi huu wa kumi kutoka COVAX FACILITY.
“Na dozi hizi ni sehemu ya Dozi Milioni 3.7 za chanjo aina ya Pfizer ambazo nchi yetu itazipata kwa awamu kutoka COVAX Facility, tayari hivi navyoongea majokofu ya baridi kali 14 yenye uwezo wa kuhifadhi chanjo zote Milioni 3.7 yameshafungwa pale jijini Dar es Salaam.
“Kupitia hii COVAX FACILITY tunatarajia kupata dozi Milioni 11.8 na pia kuna juhudi nyingine za kupata chanjo zinazoendelea ili kutimiza lengo letu la kutoa chanjo kwa asilimia 60 ya Watanzania wote,” ameeleza Msigwa.
Sambamba na hayo, amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (UVIKO-19) ambazo ni uvaaji barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka misongamano, kukaa umbali wa meta moja au zaidi, kufanya mazoezi, na kula lishe bora.