……………………………………………………………………………
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma kuwashikilia Viongozi wa Vyama vilili vya Ushirika vya Walimu, Kurugenzi Saccos na Teachers Saccos kwa tuhuma za upotevu wa fedha za michango ya Walimu Wilayani humo zaidi ya Sh Milioni 900.
Ndejembi pia ametoa maagizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Mbinga Mji na Mbinga DC kuwachukulia hatua za kinidhamu maafisa ushirika wa halmashauri hizo kwa kushindwa kusimamia vyama hivyo kwa weledi na kupelekea kupata hasara ya fedha hizo.
Naibu Waziri Ndejembi ametoa maagizo hayo wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Mbinga kwa ajili ya kuzungumza na wastaafu hao ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kuitaka Wizara ya Utumishi kukutana na wastaafu hao wa Mbinga na kutatua changamoto zao.
Akizungumza na wastaafu hao, Naibu Waziri Ndejembi amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan haitomvumilia mtu yeyote atakayejaribu kutumia fedha za wananchi wake katika kujinufaisha yeye mwenyewe ambapo ameitaka TAKUKURU kuharakisha uchunguzi wa jambo hilo ili haki ya wastaafu hao iweze kupatikana.
“Haiwezekani wastaafu wetu hawa waliotumikia Taifa lao fedha zao ziliwe, Wazee wetu hawa walichangia fedha zao kwenye Saccos hizi wakitegemea wanapostaafu wapate fedha zao, Sasa mnatuambia fedha hakuna zaidi ya Sh Milioni 900, jambo hili haliwezekani na Serikali ya Rais Samia haiwezi kukubali, TAKUKURU wachukueni viongozi wote wa sasa na zamani watueleze fedha zilipo.
TAKUKURU anzeni uchunguzi kwa viongozi wa Saccos hizi mbili, viongozi wa sasa watueleze ni kwanini waliendelea kuchukua michango wakijua vyama vina madeni, Kurugenzi Saccos wana madeni ya Sh Milioni 500, Teachers Saccos wana deni la Sh Milioni 470 haikubaliki, na viongozi wa zamani pia wachukuliwe hatua maana ubadhilifu ulianzia kwao,”Amesema Naibu Waziri Ndejembi.
Ndejembi pia ametoa maagizo kwa maafisa ushirika kuhakikisha wanasimamia vyama vya ushirika katika kujiendesha kwa weledi ili kuzuia hasara kubwa kama ambavyo imejitokeza katika vyama hivyo vilivyopo Mbinga.
“Niwatake maafisa ushirika wetu kutekeleza majukumu yenu ya kusimamia vyama hivi kwa weledi, upotevu wa fedha hizi kama Maafisa ushirika wetu mngekua makini hapa hii hali isingejitokeza, hivyo niwaagize Wakurugenzi kuwachukulia hatua za kinidhamu maafisa ushirika hawa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi,” Amesema Ndejembi.