Na Joseph Lyimo
WALIMU 100 wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamepatiwa chanjo ya Uviko-19 baada ya kuhamasishwa na Ofisa elimu ya msingi Silvanus Tairo, ambaye aliwaongoza walimu hao kupata chanjo hiyo Mji mdogo wa Mirerani.
Walimu hao walihamasika mara baada ya ofisa elimu huyo Tairo kuwaongoza kwa kupatiwa chanjo ya Uviko-19 iliyokuwa inatolewa na wataalamu wa afya wa kituo cha afya Mirerani.
Ofisa afya wa mji mdogo wa Mirerani Jovin Rweyemamu amewapongeza walimu hao kwa kupata chanjo ya Uviko-19 na kuachana na maneno potofu yaliyokuwa yanatolewa na watu ambao hawana utaalamu wa afya.
Rweyemamu amesema walimu hao wamefanya jambo sahihi kwa kupatiwa chanjo hiyo hivyo kudhihirisha kuwa wenyewe ni wataalamu wanaowasikiliza wataalamu wa afya na kufanyia kazi maelekezo yao.
“Kuchanja ni hiyari ya mtu ila walimu hawa wameonyesha mfano na kutekeleza wajibu wao kwani watu wengine huko mitaani watakaposikia walimu wamechanja nao watashiriki kwani chanjo ya Uviko-19 haina tatizo lolote,” amesema Rweyemamu.
Amewaasa watumishi wengine wa serikali washiriki shughuli hiyo ya kupatiwa chanjo ya Uviko-19 na kuepukana na maneno potofu ya mitaani yanayokatisha tamaa kuwa chanjo ina madhara.
Ofisa elimu ya msingi wilaya ya Simanjiro, Silbanus Tairo amesema walimu hao walihamasika kwa kumuona yeye akipatiwa chanjo ya Uviko-19 ila awali mwamko wao ulikuwa mdogo.
“Msikubali kusikiliza taarifa potofu za mitaani, ninyi ni wasomi changamkieni hii fursa ya chanjo kwani itakuwa ajabu mtu unaugua Uviko-19 ili halil chanjo imeletwa kwenu nanyi mkakataa kuchanja,” amesema Tairo.
Amewapongeza walimu hao kwa kumuunga mkono na kupatiwa chanjo hiyo kwani walimu 29 walipatiwa papo hapo na wengine kufuata baada ya kuona kiongozi wao amepata.
“Nawapongeza mno kwa hatua hii ya kuniunga mkono kwani wataalamu wa afya wametueleza kuwa ukipata chanjo ya Uviko-19 hata ikitokea bahati mbaya umepata maambukizi ya janga hilo madhara yatakuwa madogo,” amesema Tairo.
Amesema elimu waliyopatiwa walimu hao juu ya chanjo hiyo ya Uviko-19 na kuwaona viongozi wao wanachanja hadharani wakapata hamasa na kushiriki shughuli hiyo kwa hiyari yao.
“Natoa wito kwa walimu wengine ambao bado hawajapata chanjo ya Uviko-19, wachangamkie fursa hiyo kwani wataalamu wa afya wameshawaeleza kuwa haina tatizo lolote,” amesema Tairo.
Ofisa elimu wa kata ya Mirerani,Dinna Mbise amepongeza hatua hiyo ya uhamasishaji wa chanjo ya Uviko-19 kwani hata yeye amepatiwa ili kujikinga na janga hilo.
Mbise amesema amehamasika mara baada ya kumuona Ofisa elimu wa wilaya akiongoza shughuli ya kupata chanjo na amefarijika kupata chanjo.
“Nawaasa wale ambao hawajapata chanjo hii wafanye hivyo mara moja kwani haina tatizo na binafsi sijapata madhara yoyote tangu nilipochanja,” amesema Mbise.