Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jinsia Grace Mwangwa akizungumza na wanawake pamoja na washiriki wa kongamano la Kitaifa la Haki za Wanawake wanaoishi vijijini katika kuadhimisha siku ya mwanamke anayeishi kijijini l
Sehemu ya washiriki wa Kongamano la Kitaifa la Haki za Wanawake wanaoishi vijijini lililofanyika Mkoani Kilimanjaro wakicheza muziki katika kuadhimisha siku ya mwanamke anayeishi kijijini
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia Grace Mwangwa akizindua mwongozo wa utekelezaji wa Kampeni ya haki ya kumiliki ardhi Kwa wanawake katika kongamano la Haki ya Wanawake wa kijijini katika ardhi kwenye maadhimisho ya siku ya mwanamke wa kijijini
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kilimanjaro Hilda Lauwo akitoa salamu za Mkoa kwenye kongamano la Kitaifa la Haki za Wanawake wanaoishi vijijini lililofanyika Mkoani Kilimanjaro katika kuadhimisha siku ya mwanamke anayeishi kijijini.
………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro
Wanawake wanaoishi vijijini wamehimizwa kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili kunufaika na mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya Grace Mwangwa wakati akiwasilisha hotuba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima kwenye kongamano la kuadhimisha ya siku ya mwanamke anayeishi kijijini lililofanyika Mkoani Kilimanjaro leo tarehe 15 Oktoba, 2021.
Mwangwa amesema Serikali inatambua changamoto ya umasikini wa kipato kwa wanawake wanaojishughulisha na kilimo hususani wanaoishi vijijini na kuwa, ongezeko la uhamasihaji wa wanawake kujiunga kwenye vikundi vya kiuchumi ni ishara kwamba wanawake wengi wamenufaika na vikundi hivyo.
“Takwimu zinaonesha kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi umeongezeka kutoka vikundi 88 vyenye wanawake 1,517 mwaka 2019/20 Hadi vikundi 918 vyenye wanawake 10,708 na Maafisa Maendeleo ya Jamii wamekuwa wakiwaunganisha wanawake na fursa za mikopo pamoja na wataalamu ili kuwawezesha upatikanaji wa teknolojia za uzalishaji, uchakataji wa mazao na maonesho ya biashara” amesema Grace.
Ameongeza pia licha ya Wanawake kuwa ni asilimia kubwa ya nguvu kazi inayotegemewa na Taifa, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo kukosa kunufaika sawa ikilinganishwa na wanaume kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumiliki ardhi kwa sababu mbalimbali.
“Zaidi ya asilimia 65 ya Wanawake wako katika sekta ya kilimo na hii inadhihirisha kuwa asilimia kubwa ya mazao ya kilimo yanachangiwa na wanawake”
Amesema hata hivyo Serikali inaendelea kufanya jitihada za utekelezaji wa sera na mipango iliyopo ili kuondoa umasikini Miongoni mwa wananchi hasa wanawake ili waweze kuchangia uchumi wa nchi.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu, kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Erasto Ching’oro akielezea malengo mahususi ya Kongamano hilo, amesema linawakutanisha wanawake hususani wa vijijini kujadili Kitaifa na kuona ni Jinsi gani wanawake wanaunganishwa na kuwa na mtandao wa kibiashara na ujasiriamali, kuweza kubadilishana taarifa za mikopo na masoko pamoja na uzoefu.
Amesema lengo lingine ni kuongeza fursa na uelewa wa umuhimu wa mwanamke kupata haki ya kupata ardhi
Mwakilishi wa Wizara ya Ardhi, Magreth Mataya akizungumzia suala la mifumo ya chakula na siku hii amesema bado kuna changamoto ya uzalishaji mdogo usio na tija, kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakumba wanawake wa vijijini hivyo kuongeza uzalishaji wenye tija ni moja ya suluhisho lililofikiwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau.
Ameongeza pia upatikanaji wa haki sawa katika umiliki wa ardhi kwa wanawake wa vijijini ambao ni wazalishaji wakubwa wa chakula ni suala muhimu ili waweze kumiliki na kuwezeshwa kifedha kwa lengo la kuongeza tija katika kilimo.
Kwa upande wake mmoja wa wanawake anayeishi kijijini, Frola Mlowezi ambaye ni miongoni mwa wanawake waliopigania haki ya ardhi ameishukuru Serikali na Mashirika kwa jitihada zinazofanywa kuwawezesha wanawake wa kijijini hasa wanaojishughulisha na kilimo kwa kuweka sera na mikataba mbalimbali iliyoridhiwa kuhusu haki za Wanawake.
“Tumekuwa wadau wakubwa wa kutumia ardhi lakini tumekuwa siyo wamiliki wa ardhi ambayo ni kinyume cha sheria na. 4 ya ardhi, tunaomba tusaidiwe sheria hii iweze kuwafikia Viongozi wa ngazi za vijiji wanaoendekeza Mila kandamizi”..
Aidha wameiomba Serikali kuwashirikisha wanawake wa vijijini wakati wa mchakato wa mabadiliko ya sera ya mwaka 2000, ili mawazo yao yaingizwe kwenye sera hiyo.
Baadhi ya Wanawake pia wameiomba Serikali na Wadau kuandaa majukwaa kama hayo ya kuwawezesha wanawake kujadiliana yaende vijijini kuwafikia wanawake wengi zaidi wanaoishi huko.
Mwenyekiti wa Chama Cha wanawake wanasheria Tanzania (Tawla) Lulu Ng’wanakilala akitoa salamu za Wadau wa masuala ya Wanawake amesema kongamano hili linafanyika kwa mara ya kwanza mkoani hapa ni linatarajiwa kufanyika kila mwaka ili kuendelea kukumbushana umuhimu wa wanawake hususani wa vijijini kupata haki zao za msingi.
Amesema maadhimisho haya yanafanyika kwa kutambua nyenzo pekee ya mwanamke wa kijijini katika kujikwamua ni ardhi hivyo matukio yote yaliyofanyika ni katika kuhamasisha Jamii umuhimu wa mwanamke wa kijijini kuwa na haki ya kumiliki ardhi.
“Karibia asilimia 70 ya wazalishaji wa chakula ni wanawake wanaoishi kijijini lakini amekuwa bado akiachwa nyuma kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo kuanzia ngazi ya familia na Jamii kwa ujumla hasa kwenye maamuzi kuhusu ardhi”aliongeza Lulu.
Kongamano hilo ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mwanamke wa kijijini lilikuwa na Kaulimbiu ya “Umiliki wa Ardhi ni nyenzo muhimu ya Maendeleo ya Wanawake wa vijijini”