Kaimu Mkurugenzi Msaidizi utafiti na nyaraka Fides Shao akiwasilisha mada ya haki ya mtoto katika mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya vitendo vya udhalilishaji yaliyoandaliwa na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora katika UKumbi wa Maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.
Mratibu wa Jinsia Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Florence Chaki akiwasilisha mada ya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto katika UKumbi wa Maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.
Mwanafunzi Ummul- kulthum Mohammed akitoa mchango wake kuhusu ukatili wa watoto katika mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya udhalilishaji yaliyoyafinyika Ukumbi wa Maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.
Mwanfunzi kutoka Skuli yaKwerekwe “E” Harith Kassim akichangia mada kuhusu haki ya mtoto katika mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto yaliyoandaliwa na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora huko Mwanakwerekwe Zanzibar.
Mwanafunzi kutoka Skuli ya Kwerekwe “E” Yassir Juma akichangia kuhusu udhalilishaji wa wanawake na watoto huko Ukumbi wa maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.
Baadhi ya wanafunzi wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uelewa kuhusu vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto yaliyofanyika Ukumbi wa Maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.
Mwanafunzi Sawwah Mohammed akichangia mada kuhusu udhalilishaji kwa wanawake na watoto katika mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto yaliyofanyika Ukumbi wa Maleria Mwanakwerekwe Zanzibar.
PICHA NA FAUZIA MUSSA – MAELEZO ZANZIBAR
…………………………………………………………………………..
Na Khadija Khamis –Maelezo,
Wanafunzi nchini wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kulishughulikia suala la udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto kuwachukulia hatua za kisheria wahusika ili kuvitokomeza vitendo hivyo vinavyoathiri jamii .
Wameyasema hayo katika Ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe wakati wakipata mafunzo ya haki za binadamu kwa wanafunzi wa skuli za Sekondari na Msingi za Wilaya Magharibi “B” yaliotolewa na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora .
Wamesema vitendo vya ukatili na udhalilishaji vinafanyika mara kwa mara katika maeneo tofauti yanayowazunguka jambo ambalo linawapa wasiwasi na kuwanjima uhuru wa kucheza katika maeneo yao.
Aidha walisema sababu zinazochangia vitendo hivyo ni ukosefu wa elimu ya dini,kuporomoka kwa maadili, matumizi ya madawa ya kulevya, matumizi mabaya ya simu kwa watoto, jamii kutoshirikiana katika malezi na makuzi ya watoto,ukosefu wa ajira,ushawishi na ulaghai wa vijana pamoja na kuachiwa huru watuhumiwa wa udhalilishaji .
“Mfanyaji wa vitendo vya udhalilishaji anaachiwa kituoni kiholela, akidunda mtaani bila ya wasiwasi anaendeleza kumfanyia mtoto mwengine vitendo hivyo inatusikitisha ”, walisema Wanafunzi hao .
Akitoa mada ya udhalilishaji wa kijinsia Mwezeshaji Florence Chake , kutoka Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora alisema ukatili ni kitendo chochote kinachofanyiwa mtu na kusababisha madhara ya kimwili, kiakili,na kisaikolojia pamoja na kupewa mateso kwa kutishiwa maisha na kunyimwa uhuru.
Alifahamisha kuwa waathirika zaidi wa vitendo hivyo ni wanawake na watoto kutokana na hali zao za kimaumbile wamekuwa katika hatari ya kunyimwa haki zao kutokana na kutoweza kujitetea wanapokabiliana na vitendo hivyo .
Alieleza kuwa makundi ambayo yako katika hatari ya kufanyiwa ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ni Wanawake na Watoto, Watu Wenye Ulemavu, Wazee, Watu wenye ulemavu wa ngozi, wanaoishi na virusi vya ukimwi pamoja na Wakimbizi .
Aidha alisema Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora kazi yao ni kutoa ushauri kwa Serikali zote mbili ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuhakikisha haki za binaadamu zinalinda na kutetewa .
kauli mbiu ya Tume hiyo ni “PAZA SAUTI KOMESHA UKATILI NA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO “