Na Joseph Lyimo
WANAWAKE Mkoani Manyara, wameeleza kuwa mila kandamizi za eneo hilo zimechanjia kusababisha wanawake kuwa na changamoto ya kutopata haki ya fursa mbalimbali ikiwemo kutomili ardhi.
Mkoa wa Manyara, umetajwa kuwa miongoni mwa mikoa nchini, ambayo imeendelea kukumbatia mila kandamizi ikiwemo mfumo dume na kuwanyima wanawake fursa ya kumiliki ardhi.
Wakizungumza kwenye kuwapokea na kuwasalimia msafara wa kijinsia kuelekea siku ya Mwanamke wa Kijijini, uliotokea mkoani Mwanza na kusimama Mkoani Manyara ukielekea mkoani Kilimanjaro, baadhi ya wanawake wamepaza sauti na kuelezea kero hiyo.
Siku ya mwanamke wa kijijini, ambayo huadhimishwa kila mwaka mwezi Oktoba na mwaka huu, ikibebwa na kauli mbiu ya ardhi ni nyenzo ya maendeleo kwa mwanamke wa kijijini, pamoja na kujenga ustahimilivu kwa mwanamke anayeishi kijijini katika kukabiliana na Uviko-19.
Mkazi wa Kata ya Endasak Wilayani Hanang’ mkoani Manyara, Rose Gitagno akizungumza na msafara huo ambao lengo likiwa ni kupaza sauti kwa jamii juu ya umuhimu wa mwanamke wa kijijini kumiliki ardhi, amesema changamoto hiyo bado ipo eneo hilo.
Gitagno amesema miongoni mwa mikoa yenye changamoto juu ya kina mama kumiliki ardhi ni Mkoa wa Manyara na kueleza kuwa changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na ufinyu wa ardhi na mila na desturi zilizopitwa na wakati.
Amesema japokuwa mwanamke ni kiungo kikubwa cha malezi ya familia, linapokuja suala la umiliki wa ardhi, wanaume ndiyo wanakuwa mbele na wanawake wananyimwa hiyo haki na hata baadhi ya mila zetu, zinasema mwanamke haruhusiwi kumiliki ardhi na ikitokea baba amefariki, watu wengine wanarithi ardhi.
Mkazi wa Riroda Wilayani Babati, Magreth Bayo amesema elimu inapaswa kutolewa zaidi kwa jamii ya eneo hilo ili kuelezea umuhimu wa mwanamke kumiliki ardhi kwani mwanaume akitangulia kufa watoto na wanawake huathirika zaidi.
Bayo amesema endapo elimu ya usawa wa kijinsia ingetolewa kila mara na jamii ikatambua kuwa hakuna tofauti ya mwanamke na mwanaume kwenye majukumu ya malezi kusingekuwa na ubaguzi wa kukatazwa kumiliki ardhi.
Kiongozi wa msafara huo, Ofisa maendeleo ya jamii wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Janeth Shishila, amesema msafara huo kutoka Mwanza umepita mikoa mbalimbali nchini na kuelimisha jamii umuhimu wa mwanamke kumiliki ardhi.
Amesema shughuli kubwa za kiuchumi amekuwa akishiriki mwanamke lakini suala la matumizi ya kupanga nani aamue nini kifanyike katika ngazi ya kaya mwanamke amenyimwa haki hiyo.
“Tumepitia maeneo mbalimbali na katika msafara huu, katika maeneo ambayo tumepita tumetoa elimu ya umuhimu wa mwanamke wa kijijini kumiliki ardhi kwa maendeleo ya familia,” amesema Shishila.
Amesema katika maeneo waliyopita, wamebaini katika mikoa mingi nchini, mila kandamizi ukiwemo mfumo dume, umekuwa kichocheo kikubwa cha kuwanyima wanawake fursa ya umiliki wa ardhi.
“Maeneo mengine hawaruhusiwi kumiliki chochote katika familia na migogoro mikubwa ya ardhi inayotokana na wanawake kunyimwa kumiliki ardhi,”amesema Shishila.
Mwanasheria kutoka chama cha wanawake wanasheria Tanzania (TAWLA) Fatuma Kimwaga, amesema uwepo wa mfumo dume ni moja ya changamoto inayowanyima wanawake, fursa ya kumiliki ardhi.