Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jaji Mstaafu Thomas Mihayo (wa tatu kushoto) ambaye aikuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2022 Jijini Dar es Salaam. Wengine kutoka kushoto ni Katibu wa Chama Cha Riadha Dar es Salaam, Rahim Kassim, Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Michezo, Yusuf Singo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi, Meneja wa Chapa ya Tigo Anna Loya na Katibu Mkuu wa Chama Cha Riadha Jackson Ndaweka.
Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jaji Mstaafu Thomas Mihayo (wa tatu kushoto) ambaye aikuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2022 Jijini Dar es Salaam akiwaongoza wageni wengine kukata keki kama ishara ya uzinduzi huo. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Michezo, Yusuf Singo, Meneja wa Chapa ya Tigo Anna Loya, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi na Katibu wa Chama Cha Riadha Dar es Salaam, Rahim Kassim..
Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jaji Mstaafu Thomas Mihayo (wa tatu kushoto) ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2022 Jijini Dar es Salaam akizungumza wakati wa uzinduzi huo. Wengine kutoka kushoto ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi na Meneja wa Chapa ya Tigo Anna Loya.
Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jaji Mstaafu Thomas Mihayo (wa tatu kushoto) ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2022 Jijini Dar es Salaam. Wengine kutoka kushoto ni Katibu wa Chama Cha Riadha Dar es Salaam, Rahim Kassim, Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Michezo, Yusuf Singo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi, Meneja wa Chapa ya Tigo Anna Loya.
**************************
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon maarufu kama Kili marathon kwa mwaka 2022, yamezinduliwa leo Jijini Dar es Salaam, yakiwa ni mashindano ya 20 tangu kuanzishwa kwake.
Hafla ya uzinduzi huo, ambao yanaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya mashindano hayo maarufu Ulimwenguni ulishirikisha wadau mbalimbali wa riadha kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, ambao ulifanyika katika Hoteli ya Four Points Sheraton, mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jaji Thomas Mihayo (mstaafu) aliwapongeza wandaaji na wadhamini wa mashindano hayo kwa ushirikiano wao ambao umeyafanya mashindano hayo kuwa maarufu ndani na nje ya nchi.
Alisema Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii hapa nchini kupitia utalii wa michezo (sports tourism) jambo ambalo alisema inaunga mkono juhudi za serikali katika utekelezaji wa sera za utalii na michezo.
“Nichukue fursa hii muhimu kuwapongeza wadhamini wote wakiongozwa na mdhamini mkuu Kilimanjaro Premium Lager, Tigo ambao ni wadhamini wa 21km (Half Marathon) na Grand Malt ambao ni wadhamini wa mbio za kujifurahisha za 5km”, alisema na kuongeza bila wadhamini hao mashindano hayo yasingefana.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara kutumia fursa ya mbio hizo katika kukuza biashara zao sambamba na mapato yao kwa kuhakikisha wanatoa huduma bora na kuuza bidhaa zenye ubora wa hali ya juu huku pia akiwataka washiriki wote pamoja na watazamaji kuhakikisha wanatumia msimu huo wa Kilimanjaro Marathon kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii kama vile Mlima Kilimanjaro, mbuga za Serengeti, Ngorongoro, anzibar na vivutio vingine.
Aidha alitumia fursa ya uzinduzi huo kuwapongeza wadhamini wengine wa mbio hizo ambao aliwataja kuwa ni pamoja na Absa Tanzania, Unilever, TPC Limited, Simba Cement, Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd, Kilimanjaro Water, kampuni ya ulinzi ya GardaWorld na watoa huduma maalumu Hoteli ya Keys, Hoteli ya Kibo Palace na kampuni ya magari ya CMC.
Naye Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Michezo na Utamaduni, Yusuf Singo alitoa wito kwa wandaaji wa mashindano mengine kama hayo kuhakikisha wanaiga mfano wa Kilimanjaro marathon ambao alisema wamekuwa wakizingatia mwongozo wa Shirikisho la Riadha Ulimwenguni (IAAF) na ule wa Chama cha Riadha nchini RT hatua ambazo zimewavutia wadhamini kutoka ndani na nje ya nchi kudhamini mbio hizo.
“Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa waandaaji wa Mbio za Kilimanjaro Marathon ili kuhakikisha yanaendelea kuwa bora kutokana na umuhimu wake katika kuitangaza Tanzania na hata katika kukuza utalii kupitia michezo”, alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambaye pia ni meneja wa chapa ya Grand Malt, Irene Mutiganzi, alisema kuwa mashindano yajayo ya Kilimanjaro marathon yatakuwa ya hatua muhimu haswa ikitiliwa maanani ya kuwa chapa ya Kilimanjaro Premium Lager imekuwa mdhamini mkuu wa mbio hizo tangu kuanzishwa kwake miaka 20 iliyopita.
“Tunatarajia kuyafanya mashindano hayo ya maadhimisho ya miaka 20 kwa namna ya pekee, kwani ni ya kihistoria kutokana na ukweli ni moja ya udhamini mrefu kupitia chapa ya Kilimanjaro Premium Lager na ambayo imeifanya chapa hiyo kukua mwaka hadi mwaka”, alisema na kuongeza, tumeguswa pia na umuhimu wa mashindano haya kukuza utamaduni wa Mtanzania pamoja na utalii kwa ujumla.
Alisema kampuni ya TBL kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager imejiandaa vyema kwa maadhimisho ya Miaka 20 ya mashindano hayo maarufu.
“Tumetenga zawadi za kifedha zenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 25, ambapo washindi wa kwanza katika mbio za 42, kwa wanawake na wanaume watapata zawadi ya shilingi milioni 4 za Tanzania kila mmoja”, alisema na kuongeza katika mbio hizo za kilometa 42 kutakuwa na motisha ya ziada ya shilingi milioni 1.5 kwa kila Mtanzania atakayemaliza wa kwanza upande wa wanaume na wanawake.
Alitoa wito kwa washiriki kujiandikisha mapema wakati zoezi hilo litakapoanza rasmi Oktoba 17, 2021, kupitia anuani ya mtandano (Kilimanjaro Marathon) kupitia Tigo Pesa kwa kupiga * 149 * 20 #. “Nitoe wito kwa wanaotarajia kushiriki mbio hizi kuchangamkia fursa ya punguzo la asilimia 20 kwa wale watakaojiandikisha kuanzia Oktoba 17, 2021 hadi Januari 7, 2022, baada ya hapo watakaojiandikisha watalipa malipo yaliyowekwa na wandaaji”, alisema.
Irene pia alitoa wito kwa washiriki wa mbio za kujifurahisha za 5 km kujiandikisha mapema kwani nambari za wanaotarajiwa kushiriki kipengele hicho zinatarajiwa kupunguzwa.
Kwa upande wake, Meneja wa Chapa ya Tigo, Anna Loya, alisema Tigo imekuwa mstari wa mbele kudhamini mbio za Tigo Kili Half marathon kwa miaka saba sasa na kwamba kuwepo kwao kuendelea kuchangia kukuza vipaji vya wanamichezo na sekta ya michezo kwa ujumla hapa nchini.
“Kwa miaka mingi tumeweza kutekeleza majukumu yetu kwa kudhamini mipango mbalimbali ndani ya jamii; kwa mwaka 2022, tunatarajia kufanya makubwa zaidi haswa kupitia mradi wetu wa kuboresha mazingira (Tigo Green) ambao tuliuzindua mwaka huu na ambao umelenga kupunguza athari zinazotokana na ongezeko la joto duniani”, alisema.
Aliwapongeza waratibu, waandaaji na wadhamini wa mbio za Kilimanjaro Marathon kwa kuweza kufanikisha hadi kufikia kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake na ambayo amesema yamejenga umaarufu kwa kuwashirikisha wanariadhaa na wapenzi wa mbio hizo kutoka sehemu mbalimbali duniani.
“Nichukue fursa hii kuwahimiza wanaotarajia kushiriki mbio za Tigo Half Marathon kwa mwaka 2022, kujiandikisha mapema Tigo Pesa ili kuepuka usumbufu wa kung’ang’ania kufanya hivyo dakika za mwisho”, alishauri.
Kwa mujibu wa wandaaji wa mbio za Kilimanjaro premium lager marathon, ambazo zitafanyika Jumapili ya Februari 27, 2022, katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), usajili utafunguliwa rasmi Oktoba 17, 2021 na unafanyika kwa njia ya mtandao (www.kilimanjaromarathon .com) au kwa njia ya Tigopesa kwa kubonyeza *149*20#.
Mbio hizi zimeandaliwa na Kampuni ya Kilimanjaro Limited na kuratibiwa na Kampuni ya Executive Solutions Limited.