Katibu wa NEC Idara ya Oganaizesheni Dkt. Maudline Castico,akizungumza leo Oktoba 15,2021 jijini Dodoma wakati akizindua zoezi la ugawaji wa kadi za kielektroniki kwa wanachama wa Mkoa wa Dodoma.
Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma Pili Mbaga,akizungumza leo Oktoba 15,2021 jijini Dodoma wakati zoezi la ugawaji wa kadi za kielektroniki kwa wanachama wa Mkoa wa Dodoma.
Mjumbe wa NEC Taifa Happiness Mgongo,akielezea jinsi alivypokea kwa furaha zoezi la ugawaji wa kadi za kielektroniki kwa wanachama wa Mkoa wa Dodoma.
……………………………………………………….
Na: Alex SonnaDodoma
CHAMA cha Mapinduzi CCM kimeanza rasmi zoezi la ugawaji wa kadi za kielektroniki kwa wanachama wa Mkoa wa Dodoma zaidi ya laki tatu ikiwa ni hatua za awali ili kubaini kama zipo kasoro katika kadi hizo kabla ya kugawa kwa wanachama nchi nzima ikiwa ni ukamilishaji wa mchakato ulioanzishwa mwaka 2018.
Akizindua zoezi hilo leo Oktoba 15,2021 jijini Dodoma Katibu wa NEC idara ya Oganaizesheni Dkt. Maudline Castico ameeleza kuwa ugawaji huo utawezesha kutambua endapo zina kasoro kabla ya kuendelea na maeneo mengine.
Uandikishaji wa wanachama wa CCM kwa mfumo wa kielektroniki ulianzishwa mwaka 2018, miaka mitatu sasa ugawaji wa kadi hizo unaanza katika mkoa wa Dodoma kabla ya wanachama nchi nzima kufikiwa
“kwa hiyo tunakwenda kuzigawa hizo kwenye wilaya zote kama zoezi la kuangalia kama tutafanikiwa kiasi gani na kama kutakuwa na matatizo yoyote tutayarekebisha wakati huo tukiendelea kuchapa kadi nyingine ” amesema Dkt.Maudline
Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma Pili Mbaga amesema kuwa ugawaji wa kadi hizo utaongeza chachu kwa wana CCM kujisajili katika mfumo huo wa Kielektroniki na kutambulika na Chama
“ Zoezi hili limekuwa la muda mrefu tukisubiri kadi hizi lakini sasa zoezi hili limekamilika na leo mkoa wa Dodoma tumekwenda kupokea kadi hizi , sisi kama CCM mkoa wa Dodoma”amesema Mbaga
Naye Mjumbe wa NEC Taifa Happiness Mgongo amesema ujio wa kadi hizo ni wa muhimu kwa wanachama ambao walishapoteza imani na uongozi wa chama kutokana na kadi hizo kuchelewa kutolewa licha ya kuzilipia.