Timu ya Biashara United ya Musoma mkoani Mara imeng’ara nyumbani baada ya kuichapa mabao 2-0 Al Ahly Tripoli SC ya Libya mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Africa uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mabao ya Biashara United katika mchezo huo yalifungwa na Mshambuliaji Deogratius Judika Mafie dakika ya 39 na bao la pili limefungwa na Mshambuliaji Atupele Green kipindi cha pili kwenye dakika ya 61 ya mchezo huo ambao Biashara walitamba kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwepo nyumbani (Home Advantage).
Mchezo wa marudiano utachezwa kati ya Oktoba 22-23, 2021 nchini Libya, hivyo Biashara United wanatakiwa kulinda ushindi huo kutokana na ubora wa Wachezaji wa timu hiyo yenye mataji 12 ya Ligi Kuu nchini humo na wenye Wachezaji wengi waliosheheni kwenye timu ya taifa ya Libya
Katika hatua nyingine, wawakilishi wengine kwenye Michuano hiyo, Azam FC watacheza na Klabu ya Pyramids ya Misri katika uwanja wao wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam siku ya Jumamosi Oktoba 16, 2021.