Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Geita Gold imezipiga mkwara timu shiriki za Ligi Kuu Tanzania bara kwamba zisitegemee mteremko kwa mechi zake zitakazochezwa uwanja wake wa nyumbani wa Nyankumbu ulioko wilayani humo, ikiwemo Mtibwa Sugar utakaochezwa Jumamosi.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Geita Gold Fc, Hemed Kivuyo watacheza mechi hiyo kama nyati aliyejeruhiwa kwa sababu wamepoteza mechi mbili ambazo ni dhidi yao na Namungo na Yanga.
Kivuyo alisema mchezo dhidi ya Mtibwa ni wa kwanza kuucheza kwenye uwanja wake wa nyumbani, wanapaswa kuutendea haki uwanja wake wa nyumbani.
Pamoja na kujigamba huko, mchezaji wao, Salum Ayee ni majeruhi ambaye hali yake inaendelea kuimarika.
Kivuyo alitumia fursa hiyo kumtangaza Shafii Omary ‘JK comedian’ kuwa balozi wa timu hiyo ambako pia wanatarajia kuwatangaza mabalozi wengine hivi karibuni.
Aidha Kivuyo alitumia fursa hiyo kuwasilisha salam za pongezi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Geita, Zahara Michuzi kwa timu za Taifa za Wanawake zilizofanya vizuri katika mashindano waliyoshiriki hivi karibuni.
Alisema kupitia salam hizo, Mkurugenzi huyo ameahidi kufanikisha maendeleo ya soka la wanawake na kuahidi kujengwa uwanja kwa ajili ya soka la wanawake.
Kivuyo alisema ili kufanikisha maendeleo ya soka la wanawake kwa kubadilishana uzoefu na Chama cha Soka Ubungo (UFA).
Kivuyo alisema pia kuna wavamizi wa mitandao wameasisi tovuti feki yenye jina kama lao, jambo ambalo limeleta taharuki kwa mashabiki na wapenzi wa soka nchini kwani mtandao wao unahusika na soka pekee.
Mwenyekiti wa Ufa, Benjamin Mwakasonda, alishukuru na kupongeza ushirikiano huo utakaoleta maendeleo ya mchezo huo.
Balozi wa timu hiyo, Shafii Omary ‘JK Comedian’ alishukuru kupewa nafasi hiyo na kueleza kwamba atatoa ushirikiano zaidi kwa mashabiki wa timu hiyo.
Balozi huyo baadae aliigiza sauti za Viongozi wa nchi hii akiwemo Jakaya Kikwete, John Pombe Magufuli, baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Waziri wa Afya, Dorothy Gwajima.