Na Joseph Lyimo
Mganga Mkuu (DMO) wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dkt Aristidy Raphael amesema chanjo ya Uviko-19 ni salama iliyopitishwa na Shirika la Afya Duniani WHO hivyo watu wasihofu waitumie.
Dkt Raphael akizungumza na wadau wa maendeleo wa mji mdogo wa Mirerani amesema jamii isikubaliane na dhana potofu inayotangazwa na watu wasio na utaalamu juu ya chanjo hiyo.
Amesema watu wasio na utaalam wa afya wamekuwa wanapotosha chanjo ya Uviko-19 inavyotolewa hivyo jamii isiwape kipaumbele kwao na kuwasikiliza udanganyifu wao.
Amesema chanjo ya Uviko-19 haina tofauti na chanjo nyingine zilizoletwa nchini na kutumika ikiwemo chanjo ya polio, pepopunda na chanjo nyingine ambazo hazina madhara.
“Dhana potofu ya chanjo hiyo ya Uviko-19 imesababisha baadhi ya watu wengine ambao walikuwa na lengo la kuchanja kuhofia kupatiwa chanjo hiyo,” amesema Dkt Raphael.
Amesema pamoja na kupitishwa na WHO hata mamlaka ya nchi imefanyia utafiti na kuruhusu kutumiwa na wananchi hivyo Serikali haiwezi kukubali kuona watu wake wanapata tatizo.
“Msikubali uvumi uwaondoe kwenye mambo ya msingi, tuna watu nyuma yetu bado hawajapata chanjo hivyo ninyi ni wadau wa maendeleo nendeni mkatoe elimu kuwa chanjo ya Uviko-19 ni nzuri haina shida,” amesema Dkt Raphael.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Tanesco mji mdogo wa Mirerani Justin Abraham amesema ametoa elimu kwa wananchi wa eneo lake ambao nao wameitikia mwito wake na kushiriki chanjo.
“Mambo ya kuwasikiliza watu ambao siyo wataalamu kwetu halipo kabisa na wananchi wameshaelewa hilo na wanashiriki chanjo bila tatizo lolote,” amesema Justin.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Jafari Matimbwa amesema yeye binafsi amechanja na suala la chanjo linapaswa kupewa kipaumbele na wananchi wanatakiwa kuachana na dhana potofu zinazotolewa na watu wasio na utaalamu wa afya.
“Mtu anakwambia chanjo ni mbaya na wewe unamsikiliza ili hali hana utaalamu wowote wa afya, tunapaswa kutambua kuwa viongozi wetu hawawezi kututumbukiza kwenye shimo jamani twende tukachanje,” amesema Matimbwa.