……………………………………………………….
Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amepiga simu katikati ya hafla ya Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi na kuipongeza Timu ya Taifa ya Wanawake ya Mpira wa Miguu (Twiga Stars)leo Oktoba 12, 2021 na kutaka timu zote ziendelee kufanya vizuri ili kuitangaza Tanzania kimataifa.
Mhe. Rais amesema timu ya Twiga Stars imeliheshimisha Taifa na kwamba amekuwa akifuatilia kwa karibu timu hiyo.
“Nafuatilia hafla hii na nimemuagiza Katibu aendelee na mimi nikirejea nitawaita”. Amefafanua Mhe. Samia
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo amemhakikishia Mhe. Rais kuwa Wizara itaendelea kuboresha Michezo nchini na kwamba huu ni mwanzo wa kuelekea katika mashindano ya Dunia.
Amesema anaamini kuwa pia Timu ya Taifa ya Wanawake ya mpira wa Miguu ya U20 ya Tanzanite ambayo ipo kwenye mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia itafanya vizuri kama yalivyo madini ya thamani ya Tanzanite.
Aidha, amesema katika kipindi hiki Serikali imeweka miundombinu ya kusaidia michezo ambapo amesema kiasi cha shilingi bilioni 1.5 zimetengwa.
Katika hafla hiyo Wizara ya Sanaa, Utamaduni imetoa zaidi ya shilingi milioni 40 kwa ajili ya timu ya Twiga Stars (20m), Washindi wa mashindano ya Miss and Mr Deaf Africa 2021 waliofuzu kwenda mashindano ya Dunia (6m), Timu ya Tanzanite (10 m) na timu ya kriketi iliyoshinda nafasi ya tatu Bara la Afrika (5m) pia Makatibu wakuu wametoa 3m
Hafla hiyo imepambwa na wasanii mbalimbali wa kizazi kipya ambapo wamekonga mioyo ya watu na wadau mbalimbali wa Michezo waliohudhuria hafla hiyo.