********************************
Na Lucas Raphael,Tabora
Benki ya Tanzania Commercial Benki PLC (TCB) Mkoani Tabora imetoa msaada wa mifuko 100 ya saruji kwa shule ya seminari ya Itaga na Kanisa katoliki Ipuli kwa ajili ya kufanikisha ukarabati majengo ya shule na kumalizia kanisa hilo iliyoghalimu kiasi cha shilingi milioni 2
Akitoa msaada huo Meneja wa Tawi la Benki hiyo mkoani hapa Timony Joseph alisema benki ilifikia uhamuzi wakutoa msaada wa mifuko 100 ya saruji katika shule na kanisa ikiwa ni moja ya kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani katika suala zima la elimu na kuabudi.
Meneja huyo alisema pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali lakini shule hiyo ni wadau wakubwa wa kuweka fedha zao katika benki ya TCB hivyo saruji waliyoitoa itasaidia kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo.
Alisema miundimbinu ya shule inapokuwa mizuri inasaidia kwa wanafunzi kusoma masomo yao vizuri ikiwa pamoja na kuongeza vipaji vya elimu.
Akizungumza mara baada ya kupokea mifuko 50 ya saruji Mkuu wa Seminari ya Itaga, Gombera Padre Joseph Buhili alisema anaishuru benki hiyo TCB kwa kuamua kutoa saruji hiyo ambayo ni tendo la kiungwana la kuwajali na kuona umuhimu wa elimu.
Padri huyo alisema kwamba wameupokea msaada huo kwa mikono miwili na utatumika kwa kukarabati majengo ya shule hiyo kwa ajili ya kuwezesha watoto kusoma sehemu salama.
Aidha alisema kupatika kwa saruji hiyo kutasaidia na wadau wengine kuamua kujitokeza na kutoa msaada kama huo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule hiyo ambapo mwakani inatimiza miaka 100.
Alisema shule ya Itaga seminari inajumla ya wanafunzi 230 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita ambao wanafunzi masomo ya kiroho na kimwili ili baada ya kumaliza masomo yao wakalitumikie Taifa na jamii kwa ujumla.
Naye Paroko wa Parokia ya Ipuli Padre Ponciano Kibobera aliishukuru benki hiyo kwa kujali na kuona kanisa nalo linapaswa kupata hisani kwa kutoa mifuko ya saruji 50 yenye thamani ya shilingi milioni 1.
Alisema kwamba kanisa hilo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuingia waumini 4000 kwa wakati moja.