Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimkabidhi taarifa ya utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt Batilda Burian (kushoto) wakati wa kikao na viongozi wa mkoa wa Tabora tarehe 11 Oktoba 2021.
Wabunge wa mkoa wa Tabora wakifuatilia uwasilishaji taarifa ya utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 wakati wa kikao na viongozi wa mkoa wa Tabora tarehe 11 Oktoba 2021.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo akizungumza wakati wa uwasilishaji taarifa ya utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 wakati wa kikao na viongozi wa mkoa wa Tabora tarehe 11 Oktoba 2021.
……………………………………………………………….
Na Munir Shemweta, WANMM TABORA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka wakuu wa mikoa nchini kuhakikisha wanasimamia na kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika mikoa yao kwa kuwa kazi ya kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta ni kushughulikia migogoro ya vijiji 975.
Lukuvi alisema hayo leo tarehe 11 Oktoba 2021 mkoani Tabora akizungumza na viongozi, wabunge pamoja na watendaji wengine katika mkoa huo wakati wa ziara ya mawaziri wa kisekta katika mkoa wa Tabora.
Alisema, kamati ya mawaziri nane kazi yake kubwa ni kuangalia vijiji 975 lakini mkoa unatakiwa kusimamia kazi ya itatuzi wa migogoro ya ardhi kwa kuwa taarifa iliyopatiwa kamati inawezekana siyo taarifa ya migogoro yote ya matumizi ya ardhi katika mkoa.
” Kamati yetu ya Mawaziri nane itaendelea kwa vile vijiji 975 ila kazi ya kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi itaendelea kwa usimamizi wa wakuu wa mikoa na kama ipo sababu ya msingi ya kuondoa baadhi ya vijiji basi mkoa utainisha kwa kuwa kilichofanyika sasa hivi ni huruma ya Rais” alisema Lukuvi.
Alisema, kila mkoa Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta wanapopita wanaacha timu ya wataalamu ili kuangalia namna bora ya utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya ardhi katika vijiji kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Kila kamati yetu inapopita katika mikoa kuna taarifa mpya kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi hivyo wakuu wa mikoa wana jukumu kuhakikisha migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye mikoa yao inakoma na haijirudii tena” alisema Lukuvi.
Aliwataka wakuu wa mikoa nchini kusaidia katika suala hilo ili kero zote kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji itatuliwe bila kuumiza wananchi na migogoro hiyo lazima iishe na kama mkoa ukihitaji kusaidiwa utoe taarifa na utekelezaji wake utafanyiks kwa haraka.
Kwa mujibu wa Lukuvi kilichofanyika kumega sehemu maeneo ya hifadhi ni huruma ya Rais na kusisitiza kuwa, kama eneo ni chanzo cha maji basi eneo hilo linahitaji kutunzwa na kusisitiza kuwa ni aibu kuendelea kuwepo migogoro ya ardhi ikiwemo ile ya mipaka katika mikoa na kutaka migogoro ya ardhi kumalizwa kwa mfumo huo.
“Ni aibu kubwa kusikia kuna mpaka wa mkoa na mkoa au wilaya na wilaya kwa kuwa mwenye mamlaka ya kuweka mipaka ni rais na wakuu wa mikoa ninyi hamuendi kuanzisha mipaka mipya nendeni mkaweke alama kuwaonesha wananchi” alisema Waziri Lukuvi
Baadhi ya wabunge katika mkoa wa Tabora waliwasilisha kero za migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo yao kwa kamati ya mawaziri nane kwa kusema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakiishi kwa hofu katika maeneo yao kwa kuelezwa kuishi ndani ya hifadhi.
Mbunge wa jimbo la Kaliua Aloyce Kwezi aliiambia kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta kuwa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeweka mipaka ya hifadhi ya msitu wake wa USAWIWA hadi ndani ya mipaka ya vijiji na kuanza kuchukua hatua za kuwaondoa wananchi jambo linalowafanya kuishi kwa hofu wakati wameishi hapo kwa muda mrefu.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja aligiza taasisi zilizoko chini ya wizara yake kuacha kuwasumbua wananchi wanaoishi maeneo ya hifadhi kipindi hiki ambacho kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta wanazunguka katika mikoa mpaka pale itakapoamuliwa vinginevyo.
” Naomba tuvute subira wakati tunatekeleza maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 kuna maeneo yamesahaulika na timu imeundwa na Waziri wa Malisili na Utalii kufanya tathmini kwa baadhi ya maeneo na kutaka wananchi waachwe katika maeneo wanayoishi wasibughudhiwe” alisema Masanja.