Na Joseph Lyimo
Imeelezwa kuwa watoto 15 hadi 20 wameripotiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili na wazazi wao au ndugu zao wa karibu kila mwaka kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara.
Ofisa ustawi wa jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Mathias Focus ameyasema hayo wakati akielezea juu ya maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili Duniani yanafanyika kila mwaka mwezi Oktoba.
Focus amesema dunia kuadhimisha siku hiyo ni muhimu sana kwa kuwa inaikumbusha jamii kuwa kuna watu wanawafanyia ukatili watoto.
Amesema makundi yanayoongoza kufanyiwa ukatili ni watoto kuanzia umri wa miaka sifuri hadi miaka 15, wanawake na wazee.
Amesema ukatili unaofanywa kwa watoto mara nyingi ni kutelekezwa na wazazi wao, kupigwa, kumwagiwa maji ya moto, kutukanwa, kubakwa na kulawitiwa.
“Matukio tunayotokea ni mengi ila yanayoripotiwa ni machache na tunayomaliza kwa kujadiliana ni utelekezaji ila ya jinai tunayapeleka mahakamani,” alisema Focus.
Ametumia fursa hiyo kuionya jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi baada ya kuwa na hasira isiyo na maana yeyote.
“Mtoto anapaswa kuelekezwa na siyo kwa kutumia nguvu kwa kumpiga au kumfinya au kutumia maneno makali ambayo yanamuathiri kisaikolojia,” amesema Focus.
Amesema kuwa dunia inapoadhimisha siku ya kupinga ukatili jamii inapaswa kujitafakari na kujitathimini juu ya kutofanya vitendo hivyo.
Mkazi wa Mtaa wa Maisaka A, Mjini Babati, Yusta Shemdoe amesema chanzo cha ukatili mara nyingi ni watu kukosa roho ya Mungu ambayo ndio inaleta upendo.
Shemdoa amesema watu wanaowafanyia ukatili watoto wengi wakifuatiliwa wanaweza wakakutwa nao walikuwa wanafanyiwa hivyo na sasa wanalipiza kisasi.
Mkazi wa mtaa wa Negamsi Mjini Babati, Paul Mshana amesema Serikali imekuwa ikiwahukumu watu wanaolawiti na kubaka watoto ila wanaowafanyia ukatili wa kuwatukana, kuwafinya na kuwakebehi hawachukuliwi hatua.
“Inabidi hatua zichukuliwe dhidi ya wote wanaowafanyia watoto matukio hayo ya ukatili na mwisho wa siku tabia hiyo itapungua kama siyo kumalizika kabisa,” amesema Mshana.
Hata hivyo, kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Kamishina msaidizi (ACP) Merrisone Mwakyoma amesema wanaendelea kutoa elimu kwa jamii ya eneo hilo ili waachane na matukio hayo ya ukatili.
“Vitendo vya ukatili kwa watoto siyo matukio mazuri, tumekuwa tukiwaelimisha juu ya kuachana na matukio hayo yasiyo na tija,” amesema kamanda Mwakyoma.