Mwenyekiti wa Vituo vyote Kanisa Halisi la MUNGU BABA Ndani na Nje ya Nchi ya Tanzania, BABA Halisi akizungumza katika Ibada ya Uzalishaji, kutangaza pamoja na kuuza bidhaa iliyofanyika Makao Makuu ya Kanisa la MUNGU BABA Jijini Dar es Salaam.
Waumini wa Kanisa la MUNGU BABA wakishiriki Ibada ya Uzalishaji, kutangaza pamoja na kuuza bidhaa iliyofanyika Makao Makuu ya Kanisa hilo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waumini wa Kanisa la MUNGU BABA wakiuza na kutangaza bidhaa zao baada ya kumalizika kwa Ibada iliyofanyika Makao Makuu ya Kanisa hilo Jijini Dar es Salaam.
……………………………………………………………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Jamii imetakiwa kushiriki ibada ya kweli inayofundisha kufanya kazi au shughuli mbalimbali za kimaendeleo ambazo ni rasmi zinazomuwezesha mtu kupata kipato bila kufanya matendo maovu.
Akizungumza katika ibada maalumu ya Uzalishaji, kutangaza na kuuza iliyofanyika Makao Makuu ya Kanisa la MUNGU BABA Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa vituo vyote vya Kanisa hilo Ndani na Nje ya nchi ya Tanzania, BABA Halisi, amesema kuwa mtu asiyefanya kazi asilie, kwani Mwenyezi Mungu anamtaka kila binadamu kufanya kazi ndipo apate riziki au mahitaji yake.
BABA Halisi amesema kuwa baadhi ya dini zimekuwa zikiwafundisha wafuasi wake kwamba kupata ziriki au mahitaji ni kwa njia ya maombi na miujiza pekee, jambo ambalo sio kweli.
“Maombi pekee yanaweza kumfanya mtu kupata chakula, mavazi, malazi na mahitaji mengine yoyote anayohitaji mwanadamu ikiwemo kupata mume au mke bila kufanya kazi ? kitu ambacho sio kweli “ alihoji BABA Halisi.
Amesema kuwa zipo baadhi ya dini au madhehebu yamefunuliwa kuelewa kuwa hakuna kutumaini maombi au miujiza ili binadamu apate riziki au mahitaji yake yoyote bali njia pekee ni kufanyakazi kwa juhudi na maarifa, huku ukimtanguliza Mungu mbele kwa ajili ya shukurani kwake unapopata.
BABA Halisi amesema kuwa Adamu akiwa bado kwenye kitanga cha mkono wa Chanzo cha mema na mazuri , aliambiwa azalishe, atiishe, aongezeke na amiliki kila kilichoumbwa (mwanzo 1:28).
“Katika yote aliyoambiwa hapo juu la kwanza aliloambiwa Adamu ni kuzalisha,baada ya Adamu kutoka kwenye kitanga cha Mkono wa Muumba wa vyote, Wote na Yote na kuonekana wazi, aliambiwa pia azalishe kwa maana ya kulima na kutunza Bustani ya Edeni (Mwanzo 2:7-15)” amesema BABA Halisi.
Amefafanua kuwa kulima na kutunza bustani ina maana kazi yoyote ya halali unayoifanya ni kulima na kutunza, hiyo ndiyo ibada ambayo Chanzo Halisi ambapo watumishi wa Mungu walipewa kusimamia shamba lake (Mathayo 21:33-40).
Kanisa Halisi la MUNGU BABA ni miongoni mwa Makanisa ambalo linaamini kuwa maombi au miujiza siyo njia ya Binadamu kuweza kupata mahitaji ya uhakika ya kila kitu, bali kufanyakazi au uzalaishaji ndiyo njia halisi ambayo inaweza kumfanya Binadamu kupata takwa lake.
Kutokana na kuamini hivyo Kanisa Halisi la Mungu Baba limekuwa linahimiza waumimi wake kuzalisha kwa kuwapa kauli mbiu katika kila ibada kwamba “Ibada ni uzalishaji, Uzalishaji siyo aibu”.
Ili kuhamasisha waumini wake kufanya kazi za uzalishaji kanisa mara kwa mara limekuwa likifanya ibada maalumu inayohusiana na dhana hiyo.
Katika mwendelezo wa dhana hiyo, Kanisa hilo limekuwa likiandaa ibada maalum ya Mauzo na Uzalishaji, ambayo imefanyika leo Jumapili, Oktoba 10, 2021 kwa kalenda ya Kanisa hilo ni (26 Abu Vol.2), ambapo Wamekaribisha bila ubaguzi wa aina yoyote Wazalishaji na Wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuuza na kutangaza bidhaa zao.
Kuanzia siku kanisa Halisi la MUNGU BABA lilipoanza kufundisha kuwa Ibada ni Uzalishaji, kulitokea maswali ndani na nje ya Kanisa! Walioko ndani ya Kanisa walikutana na kile alichofanya Yesu alipoingia ndani ya Hekalu akakuta Meza za wafanyabiashara na kuzipiga mateke huku akisema nyumba ya Baba yake ni ya sala (Mathayo 21:12-13).
Hawakujua kuwa Yesu alikuwa na maana ya kufukuza wapangaji wabaya ndani ya Moyo, ambao wanatakiwa kufutika ili Mzalishaji azalishe utajiri kwa amani, wapangaji hao ni wale walioandikwa katika Marko7:21-23.
Walioko nje ya kanisa wao waliona ni mafundisho yasiyoeleweka kwa kuwa walifundishwa kuwa Kanisani ni mahali pa kwenda kumlilia MUNGU wakati wa shida na taabu peke yake.
Hawakukumbuka kuwa, wakati wa kuumba kwa mara ya kwanza, MUNGU BABA yaani chanzo cha mema na mazuri, alianza kwa kuweka heshima na utajiri ndani ya ule Moyo wa Mwanzo aliouengua kushoto kwake (Mithali 3:16).