Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa la Serikali kuhusu msimamo wa Tanzania kwenye majadiliano ya Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi leo Septemba 11, 2021 jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, MheAbdallah Ulega na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga akitoa utambulisho wakati wa kutoa Tamko la Serikali kuhusu msimamo wa Tanzania kwenye majadiliano ya Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi leo Septemba 11, 2021 jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, MheAbdallah Ulega akizungumza wakati kutoa Tamko la Serikali kuhusu msimamo wa Tanzania kwenye majadiliano ya Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi leo Septemba 11, 2021 jijini Dodoma.
Washiriki wakiwa katika Kikao kazi cha maandalizi ya mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika jijini Glasgow nchini Uingereza Oktoba 31 hadi Novemba 12, 2021.
Afisa Mazingira Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Fred Manyika akiwasilisha Msimamo wa Nchi katika Kikao kazi cha maandalizi ya mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika jijini Glasgow nchini Uingereza Oktoba 31 hadi Novemba 12, 2021.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo (katikati) akiwa katia picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Mifugo, Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Mazingira, Dkt. Andrew Komba (kushoto) na Mkurugenzi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Macocha Tembele.
………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo amesema, Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 serikali imetenga kiasi cha shilingi bilion 362 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kuhimili athari za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kauli hiyo ameitoa leo Oktoba 10,2021 jijini Dodoma wakati akitoa Tamko la Serikali kuhusu msimamo wa Tanzania kwenye majadiliano ya Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.
Aidha amesema Tanzania pia imetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kujenga kuta za bahari kwa ajili ya kuzuia mmomonyoko wa fukwe katika maeneo ya barabara ya Barack Obama na cho cha mwalimu nyerere jijini Dar es salaam na kisiwa Panza Zanzibari.
“Miradi hiyo inatekelezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, nishati, misitu, viwanda na TEHAMA pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi,”amesema Jafo
Amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zimeilazimu Serikali ya Tanzania kutumia asilimia mbili mpaka tatu ya Pato la Taifa katika kukabiliana na madhara hayo.
“Fedha hizi ni nyingi sana ukizingatia hali ya uchumi wa Tanzania na vipaumbele vya Serikali katika kuleta maendeleo kwa watu,” amefafanua
Pia amesema kuwa mchango wa uzalishaji wa gesi joto utokanao na shughuli za kilimo ni mdogo katika nchi zinazoendelea ukilinganisha na nchi zilizoendelea na hivyo kumekuwa na maoni kinzani kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea kuhusu kujumuisha sekta ya kilimo katika sekta zinazotakiwa kupunguza uzalishaji wa gesijoto.
Hata hivyo amesema kuwa nchi zinazoendelea kama Tanzania ili ziweze kujiimarisha kwa ufanisi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi, zinahitaji kujengewa uwezo katika kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye Mkataba na Makubaliano ya Paris.
“Msimamo wa Tanzania katika suala hili ni kuzitaka nchi zilizoendelea pamoja na mashirika ya kimataifa kutilia mkazo suala la kujenga uwezo wa nchi zinazoendelea ili ziweze kutoa mchango wake katika kupunguza uzalishaji wa gesijoto duniani,” amesema Waziri Jafo.
Aidha, kwa mujibu wa Mkataba huu, nchi zilizoendelea ziliahidi kutoa kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 100 kila mwaka ifikapo mwaka 2025 ili fedha hizi ziwezeshe nchi zinazoendelea kama Tanzania kuweka mipango na mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.
Hivyo amesema msimamo wa Tanzania katika suala hili ni kuzitaka nchi zilizoendelea kutimiza wajibu wao wa ahadi ya kutoa fedha hizi kama ilivyokubaliwa.
Kuhusu mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Jafo alifafanua kuwa Makubaliano ya Paris yanaitaka kila nchi mwanachama kuandaa Mchango wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo Tanzania iliwasilisha mchango wake kwenye sekretarieti ya Mkataba tarehe 30 Julai 2021.
“Msimamo wa Tanzania katika suala hili ni kwamba Mkutano huu ufikie maamuzi yatakayowezesha upatikanaji wa fedha za kuwezesha nchi zinazoendelea kutekeleza michango yao na kwamba mapitio ya michango hiyo yafanyike kila baada ya miaka mitano,” amesema
Aidha amefafanua kuwa suala la upunguzaji wa gesijoto kwenye uso wa dunia halina budi kufanyika ili ongezeko la joto liwe chini ya nyuzi joto 20C na pia juhudi za ziada zinahitajika ili ongezeko lisivuke nyuzi joto 1.50C kwa ajili ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema kuwa Makubaliano ya Paris kwenye kipengele cha 6 yanatoa fursa ya nchi mbalimbali kushirikiana kwenye upunguzaji wa gesijoto kwa kutumia mbinu ya biashara.
Hivyo Msimamo wa Tanzania ni kwamba nchi inayouza ziada ya upunguzaji isijumuishe kiwango kilichouzwa kwenye orodha yake ya upunguzaji ili kusitokee kuhesabiwa mara mbili kwani nchi iliyonunua ziada hiyo ndiyo itaweka kiwango hicho kwenye orodha yake ya upunguzaji gesijoto.
Mkutano huu unafanyika katika kipindi ambacho shirika la moja wa mataifa la hali ya hewa Duniani limetoa taraifa inayothibitisha kuwepo kwa ongezeko la joto katika uso wa Dunia na kusababisha athari za mabadiliko ya tabianchi katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania huku Mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa Mkataba wa umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi unatarajia kufanyika Oktoba 31, hadi Novemba 12,2021 Jijini Glasgow nchini Scotland