Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa ameshika ujumbe wenye maua aliopewa katika Mkutano wa Kimataifa wa Amani uliofanyika Roma,Italia. Mkutano hubo umefungwa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis akiwa na viongozi wengine wa kiroho kutoka katika madhehebu mbalimbali duniani wakati wa kufunga Mkutano wa Kimataifa wa Amani uliofanyika Roma,Italia
*********************************
Tanzania imezikumbusha Nchi zilizoendelea kutekeleza kikamilifu ahadi ya kutoa fedha kwa Bara la Afrika kwa lengo la kusaidia kukabiliana na athari hasi za mabadiliko ya tabianchi jambo litakaloziwezesha nchi hizo kutumia rasilimali kidogo ilizonazo katika kupambana na janga la UVIKO – 19.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, ameyasema hayo katika Mkutano wa Kimataifa wa Amani unaofanyika Roma,Italia na kufafanua kuwa katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu Mazingira uliofanyika mwaka 2015 jijini Paris, Ufaransa, nchi zilizoendelea ziliazimia kutoa kiasi cha dola bilioni 100 kwa nchi zinazoendelea kusaidia kukabiliana na athari hasi za mabadiliko ya tabia nchi ahadi ambayo mpaka sasa haijatekelezwa kikamilifu jambo linalolazimisha nchi za Afrika kutumia rasilimali kidogo ilizonazo huku likikabiliwa na janga la UVIKO -19.
Aidha, katika Mkutano huo Tanzania imeendelea kupaza sauti kuhusu kuzingatia usawa katika upatikanaji na usambazaji wa chanjo ya UVIKO – 19 hususani katika Bara la Afrika ili kuleta usawa,haki na uwajibikaji katika kupambana na ugonjwa huo hatari ambapo katika Bara la Afrika ni asilimia mbili hadi tatu ya wananchi wake waliopata chanjo jambo ambalo ni tofauti kwa nchi zilizoendelea ambapo wananchi wake wengi wameshapata chanjo mpaka hivi sasa.
Katika mkutano huo, suala la Umoja wa Afrika (AU) kujumuishwa katika Kundi la Nchi 20 zilizoendelea kiuchumi duniani maarufu kama G20, liliibuliwa na Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Prof. Jeffrey Sachs, na kutaka kuundwa kwa kundi jipya la G21 ili kutolitenga Bara hilo ambalo lina idadi kubwa ya watu na kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kijamii,kiuchumi na kiusalama.
Katika hafla ya kuhitimisha Mkutano huo wa Kimataifa wa Amani iliyohudhuriwa pia na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ambaye ametoa wito wa kunyamazisha silaha katika maeneo mbalimbali yenye machafuko duniani ili kuleta amani na kwamba fedha zinazotumiwa kununulia silaha zielekezwe katika mapambano ya ugonjwa wa UVIKO -19 ikiwemo suala la utoaji wa chanjo.