Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akikabidhi Hundi ya mkopo wa sh. milioni 215 kwa vikundi vya Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Mkoani Mbeya kutokana na mapato ya Halmashauri.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akipokea zawadi kutoka kikundi cha “Bamboo Group” cha kata ya Isongolo, Rungwe walizotengeneza wao wenyewe kutokana na bidhaa za mianzi, alipowatembelea katika ziara yake Mkoani Mbeya.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akikabidhi mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Swaya kuunga mkono juhudi za wananchi hao walioanzisha ujenzi huo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akishiriki ujenzi wa Kituo cha Afya katika kata ya Swaya, Halmashauri ya wilaya ya Rungwe kwa kupandisha kipande cha mbao, ikiwa ni kuwahamasisha wananchi kushiriki shughuli za Maendeleo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na kikundi cha “Bamboo Group” katika kata ya Isongolo, kinachojishughulisha na kutengeneza bidhaa za mianzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, mkoa wa Mbeya.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akitoa zawadi Kwa watoto wa Kituo cha malezi ya watoto Igogwe, Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya alipotembelea Kituo hicho kukagua utekelezaji wake.
……………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu RUNGWE
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoa elimu ya kutosha kwa vikundi vinavyonufaika na mikopo ya kuwawezesha kiuchumi ili viweze kujikwamua.
Mhe. Mwanaidi akikabidhi mkopo wa sh 215 kwa vikundi 32 vya Halmashauri ya Wilaya Rungwe amesema vikundi hivyo vikipata elimu vitasaidia kuleta Maendeleo ya kiuchumi kwa wao wenyewe na Taifa.
“Tusisite kuwapa mikopo wananchi wanaojitolea kujiunga katika vikundi tuwape elimu ya kutosha kadiri ya mipango yao na mahitaji yao ili waweze kujiendeleza na kuhakikisha hawakwami katika mipango yao na wanasonga mbele” alisema Mhe. Mwanaidi.
Mhe. Mwanaidi ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kwa kusimamia vizuri mapato na kutenga fedha za mkopo kuwawezesha wananchi na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kujiunga vikundi ili wanufaike na mikopo hiyo.
Awali akiwasilisha taarifa ya mikopo hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe alisema katika fedha hiyo, sh. milioni 60 ni kutokana na mapato ya ndani na sh. milioni 155 ni sehemu ya fedha za marejesho ya mikopo.
Aidha, Mchau Ameongeza kuwa Halmashauri kwa kushirikiana na Wadau wamekuwa wakitoa mafunzo kwa vikundi hivyo ili kuhakikisha mikopo inatumika ipasavyo na kurejesha kwa wakati ili wananchi wengine wanufaike.
Mchau amesema kwa robo ijayo ya mwaka, vikundi vitakavyopewa kipaumbele kwenye mikopo ni vile vitakavyokuwa na mweleko wa kuwa na viwanda na kutoa ajira kwa wengine ikiwemo kikundi Cha “Bamboo” kinachotarajiwa kuanza uzalishaji wa vijiti vya kusafishia meno (toothpick) kilichopo kata ya Isongolo Wilayani hapo.
“Kwenye mfuko wetu wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu tuna jumla ya sh. milioni 1.8 zipo katika mzunguko, tulishakaa na kukubaliana kuwa ifikie hatua tuwe na vikundi vya Wanawake na vijana vyenye kuleta tija kwa kuwa kampuni, vinavyoweza kukopesheka kwenye benki lakini pia kutoa ajira na kusaidia katika uchumi wetu”
Kwa upande wao baadhi ya wanavikundi waliopata mkopo huo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuhakikisha wanawainua kiuchumi kwani mikopo hiyo inawasaidia kuongeza mitaji ya shughuli zao hivyo kuongeza uzalishaji na kuweza kutunza familia zao.
“Kikundi chetu kina ng’ombe wa maziwa na tuna uwezo wa kutoa Lita 47 kwa siku, leo hii tumepata mkopo mkubwa sh. mil 22 tunategemea kuongeza ng’ombe zaidi na hapo baadaye tunatarajia kuwa na kiwanda cha kusindika maziwa na kuajiri vijana wengi” amesema Kaimu Juma mmoja wa wanufaika.